Arsenal itaangushia Man City kichapo inavyodaiwa? – Taifa Leo


ARSENAL wanapigiwa upatu kushinda mechi kubwa dhidi ya Manchester City licha ya mtihani mkali unaotarajiwa kutoka kwa mabingwa hao watetezi ugani Emirates, Jumapili usiku.

Kwa mujibu wa kompyuta maalum ya kuchanganua data Opta, vijana wa kocha Mikel Arteta wanaokamata nafasi ya pili wamepewa asilimia 46.2 kukomoa masogora wa Pep Guardiola (nambari nne) ambao wameonekana kufufuka kwa majuma machache sasa.

City wamepewa na Opta asilimia 28.1 ya kuzima wanabunduki wa Arsenal, huku asilimia 25.7 iliyosalia ikiwa ni uwezo wa mechi hiyo kutamatika bila mshindi.

Arsenal na City wanaingia mechi hiyo ya raundi ya 24 wakiwa wametoka sare mara mbili mfululizo walipokutana Machi 3, 2024 (0-0) na Septemba 22, 2024 (2-2) ugani Etihad.

Ziara ya mwisho ya City ugani Emirates iliishia kuwa kilio baada ya Gabriel Martinelli kuwazamisha 1-0.

Arsenal wanatarajiwa kukaribisha kipa nambari moja David Raya kikosini baada ya kumkosa akihisi usumbufu wa misuli katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Girona, mnamo Jumatano.

Kipa wa Arsenal, David Raya (jezi nyeusi), adaka boli kukwepa straika Haaland (jezi buluu) wa Man City, mechi ya EPL uwanjani Emirates mnamo 2023. PICHA | AFP

Mabeki Jurrien Timber, William Saliba na kiungo Declan Rice pia wanarejea kikosini baada ya kupumzishwa dhidi ya Girona. Kinachosalia kufanya Arteta kujikuna kichwa ni idara ya mashambulizi.

Kai Havertz, ambaye mara si haba amekosolewa na mashabiki kwa kupoteza nafasi tele, ataongoza mashambulizi ya Arsenal. Mvamizi Leandro Trossard anatarajiwa kutegemewa katika safu hiyo.

Erling Haaland na Phil Foden ni baadhi ya washambulizi matata wa City ambao Arsenal hawana budi kuwaweka kimya dakika zote ili kuepuka masaibu.

Naye Ruben Amorim atatumai kushinda mechi mbili mfululizo ligini kwa mara ya kwanza katika mchuano wake wa 13 wakati vijana wake wa Manchester United wataalika Crystal Palace ugani Old Trafford.

Nao Tottenham Hotspur watalenga kushinda Brentford nyumbani na ugenini kwa mara ya kwanza katika msimu mmoja watakapozuru uga wa Gtech.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*