Manchester United wameangukia pua nyumbani dhidi ya Crystal Palace kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuchapwa 2-0 katika mechi ya raundi ya 24 mnamo Jumapili, Februari 2, 2025.
Mashetani wekundu wa United waliokubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Palace ugani mwao Old Trafford msimu 2023-2024, walipewa dozi maradufu kupitia magoli ya Jean-Philippe Mateta yaliyopatikana dakika ya 64 na 89.
Eze Eberechi aliyeingia nafasi ya Daichi Kamada dakika ya 61, alichota frikiki safi na mpira ukaramba Maxence Lacroix kichwa na kupiga chenga kipa Andre Onana, ukagonga mwamba kabla ya kuwekwa ulikostahili nyavuni na Mateta dakika ya 64.
Pande zote zilikuwa zimepoteza nafasi kadhaa nzuri kabla ya straika huyo Mfaransa kufungua ukurasa wa magoli.
Mateta kisha alizamisha chombo cha United dakika ya 90 kutokana na pasi murwa kutoka kwa Daniel Munoz.
Matokeo hayo yanamaanisha kuwa United sasa imeshindwa kupata bao dhidi ya Palace katika michuano minne mfululizo, ikiwa ni mara ya tatu katika historia yao baada ya 1981 na 1983 dhidi ya Arsenal.
Ni ushindi wa tatu mfululizo wa Palace ugenini kwa mara ya kwanza tangu Aprili na Mei 2019.
United walikuwa na motisha tele wakialika Palace ugani Old Trafford baada ya kupepeta Rangers 2-1 na Steaua Bucharest kwenye Ligi ya Uropa na kubomoa Fulham 1-0 ligini. Palace walikuwa wakiuguza kichapo cha 2-1 kutoka kwa Brentford ligini.
Nao Tottenham waliangamiza Brentford nyumbani na ugenini kwa mara ya kwanza kabisa katika msimu mmoja kwa kulemea wenyeji wao 2-0 kupitia mabao ya Vitaly Janelt (alijifunga dakika ya 29) na Pape Matar Sarr aliyemegewa pasi safi kutoka kwa Son Hueng-min dakika ya 87.
Palace ni nambari 12 kwa alama 30 wakifuatiwa na Manchester United (29) na Tottenham (27). Tottenham wameruka kutoka nafasi ya 16 hadi 14 baada ya ushindi huo wao wa kwanza katika mechi saba ligini.
Brentford wanapatikana nafasi ya 11 kwa alama 31 kwenye ligi hiyo ya klabu 20 inayoongozwa na Liverpool kwa pointi 56.
Leave a Reply