Si salama kwa waliotekwa nyara wakaachiliwa, wasema Subaru zinawaandama – Taifa Leo


WATETEZI wa haki za kibinadamu ambao ni wakazi wa Kitengela, Bob Njagi, Aslam Longton na Jamil Longton hawaishi kwa amani tangu walipoachiliwa huru baada ya kutekwa nyara 2014.

Mnamo Jumapili, watatu hao walisema wanahangaishwa kila mara kwa kutishwa kwa njia ya simu na watu wasiowafahamu.

Bw Njagi aliyetekwa nyara na ndugu wawili wa Longton mnamo Agosti 19 na kuzuiliwa kwa siku 32, walisema gari moja linaloshukiwa kutumiwa na polisi limekuwa likimfuata kwa siku kadhaa.

“Tangu tuachiliwe huru, tumekuwa tukifuatwa na watu ambao tunaamini ni maafisa wa usalama. Niligundua kuwa gari aina ya Subaru Outback yenye nambari ya usajili KDP 044J na vioo vyeusi limekuwa likifuatia kila asubuhi nikifanya mazoezi ya viungo Kitengela,” Bw Njagi akasema.

Gari hilo hilo lilikuwa likimfuata kwa siku kadhaa akienda sokoni, tishio ambalo alisema limemlazimu kuhama makazi mara tatu sasa katika jaribio la kulikwepa gari hilo la Subaru.

“Mawasiliano yetu kwa njia ya simu pia yanadukuliwa na kurekodiwa. Hatuwezi kuendelea na shughuli zetu za kawaida kwa utulivu. Kwa mfano, binafsi nimelazimika kuhama kutoka mahala ambapo nilikuwa nikiishi, siyo mara moja, bali mara mbili. Hata tunapotembea, huwa tumejawa na wasiwasi kuhusu usalama wetu,” Bw Njagi akasema.

Kutokana na hali hiyo, watatu hao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kitengela mnamo Januari 29 kwa nambari ya OB 44/19/1/2025 NA 55/29/1/2025. Lakini Bw Longton na kakake walidai kuwa maafisa wa polisi katika kituo hicho waliwadhulumu.

“Kisa hiki kiliripotiwa kwa Afisa Msimamizi (OCS) wa Kituo cha Polisi cha Kitengela na Kamanda wa Polisi Kajiado lakini hakuna hatua ilichukuliwa kulinda usalama wetu,” wakasema.

Bw Njagi, Longton na kakake, wanaamini kuwa kesi iliyoko mahakamani ambapo serikali imeshtakiwa kwa visa vya watu kutekwa nyara na kuuawa, na ambapo wao ni mashahidi, ndio imesababisha madhila wanayopitia.

Jamaa za Justus Mutumwa na Kalani Mwema, waliotoweka katika eneo la Mlolongo kati ya Desemba 16 na 17, 2024, pia wameelezea kuhangaishwa.

Duncan Kyalo, kakake Mutumwa, ambaye mwili wake ulipatikana katika makafani ya Nairobi Funeral Home, alisema tangu kakake afe amekuwa akipigiwa simu na watu asiowajua.

Anasema watu huo walimwonya akome kujadili suala la kutoweka kwa kakake na kifo chake, la sivyo watamkujia.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*