NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki sasa ndiye nyapara wa kuvumisha serikali katika ukanda wa Mlima Kenya akionekana kuanzisha mikakati ya kulemaza umaarufu wa mtangulizi wake Rigathi Gachagua eneo hilo.
Profesa Kindiki ameaminiwa kukwea mlima telezi wakati ambapo wengi kutoka eneo hilo wanaonekana kuasi utawala wa Kenya Kwanza ambao waliupigia kura mnamo 2022.
Tangu kung’olewa kwa Bw Gachagua kwenye wadhifa wake mnamo Oktoba mwaka jana, kiongozi huyo amekuwa akiendeleza siasa kali ya kuipiga vita serikali miongoni mwa jamii ya eneo hilo.
Hata hivyo, baada ya kudaiwa kuhepa eneo hilo, Profesa Kindiki sasa anaonekana kuanza misururu ya mikutano akilenga kuondoa dhana kuwa Rais William Ruto hana ufuasi wowote Mlima Kenya tena.
Mara ya mwisho ambapo Rais William Ruto alizuru eneo la Mlima Kenya ni mnamo Novemba 16, 2024 ambapo alikuwa kwenye hafla ya kutawazwa kwa Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Embu Peter Kimani.
Hii ina maana kuwa Rais hajakanyaga Mlima Kenya kwa siku 80 na akiwa kwenye hafla hiyo, alizomewa na raia ambao walipinga vikali baadhi ya sera za serikali alizokuwa akieleza mkutanoni.
Baada ya kuonekana kukwepa eneo hilo kisiasa, Profesa Kindiki Jumamosi aliwaongoza baadhi ya wanasiasa wakuu, kuwachangishia wahudumu wa bodaboda Kaunti ya Embu.
“Lengo kuu la serikali ni kuweka pesa zaidi kwenye mifuko ya raia na kuimarisha hali yao ya maisha. Hii ndiyo maana tunajikakamua kwenye kila sekta kuhakikisha kuwa tunapiga hatua zaidi kiuchumi,” akasema Profesa Kindiki.
Kama njia ya kuwadhihirishia wakazi kuwa yeye ni mmoja wao, naibu rais alikwepa kutumia magari yake ya kifahari huku akiendesha bodaboda na kutangamana na raia. Hii ni kati ya mbinu zilizompa Rais Ruto uungwaji mkono sana kutoka kwa akina yakhe 2022.
Kwenye hafla hiyo, aliandamana na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na mshauri wa rais kuhusu masuala ya kiuchumi Moses Kuria. Pia alikwepo Gavana wa Embu Cecily Mbarire na wabunge wa eneo hilo ambao wamekuwa mwiba kwa siasa za Bw Gachagua.
Ziara ya Profesa Kindiki Embu ilikuja siku chache tu baada yake kupiga kambi eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri ambapo alimtaka Bw Gachagua kusitisha siasa kali ambazo zinawachochea wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya serikali.
“Wakati wa siasa ukifika si tutapiga siasa. Kuna watu walikuwa wanataka tuwachane na kazi tupige siasa lakini hatutakubali hilo,” akasema Profesa Kindiki.
Wakati wa ziara Nyeri alisema serikali itatumia Sh17 bilioni kuimarisha barabara za eneo la Mlima Kenya. Pia alisema Sh8.7 bilioni zitatumika kuunganisha umeme ukanda huo.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo, Profesa Kindiki ana mlima wa kukwea iwapo atakuwa akilenga kudumisha umaarufu wa serikali Mlima Kenya.
“Inategemea sana siasa ambazo Profesa Kindiki atacheza eneo la Mlima Kenya na mwenyewe lazima ajitahidi ili kumridhishia Ruto kuwa bado anatosha kuwa mgombeaji mwenzake wake mnamo 2027,” akasema Bw Bigambo.
Mchanganuzi huyo anasema Profesa Kindiki ana changamoto kubwa sana kwa sababu pia lazima aonyeshe yeye ni tegemeo ya maeneo mengine ili kudumisha wadhifa wa unaibu rais 2027.
“Profesa Kindiki anakabiliwa na mtihani mgumu kuelekea 2027 na binafsi kwa sasa namwona lengo lake la kugawa baadhi ya kura za eneo hilo na pia kuhakikisha hajaondolewa na Rais kisha mgombeaji mwengine achukuliwe mnamo 2027,” akaongeza.
Wiki jana, Profesa Kindiki alikutana na viongozi kutoka ngome yake ya kisiasa ya Tharaka-Nithi kule Karen ambapo alichemkia matamshi ya Bw Gachagua kuwa lengo lake ni kumfanya Rais awe kiongozi wa muhula moja.
Siku chache kabla ya mkutano huo, aliandaa mkutano na viongozi wa kisiasa, wasomi na wafanyabiashara katika makazi yake hayo ambapo alisema kuwa eneo hilo halitatengwa kisiasa kutokana na maasi yanayoendelezwa na kundi la Bw Gachagua.
Kwa mujibu wa Profesa Macharia Munene, wakazi wa Mlima Kenya kwa sasa wanajiona wapo upinzani kutokana na ahadi nyingi kukosa kutimizwa ndiposa itakuwa vigumu kwao kuunga Rais mnamo 2027.
“Shida si Gachagua kwa sababu maasi hayo yalianza hata kabla ya kufurushwa kwake serikalini. Hoja ni miradi ambayo Profesa Kindiki anazungumzia itatekelezwa na kuwadhihirishia wakazi kuwa serikali inawafanyia kazi?” akasema Profesa Munene.
Msomi huyo anasema kuwa eneo hilo limeridhika kuwa halitaki urais mnamo 2027 na iwapo kutakuwa na mwaniaji bora kutoka upinzani 2027, basi Profesa Kindiki ataambulia pakavu kwenye jitihada zake za kupata kura nyingi.
Leave a Reply