DAR ES SALAAM, Tanzania
TANZANIA imethibitisha kuuawa kwa wanajeshi wake wawili katika mapigano yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Jeshi la Ulinzi la Tanzania (TPDF) lilieleza kuwa wawili waliuawa katika mashambulio yaliyotekelezwa na wapiganaji wa M23 katika miji ya Sake na Goma Januari 24 na 28, mtawalia.
Wengine wanne walijeruhiwa katika mashambulio hayo, TPDF iliongeza.
Baada ya ufichuzi huo kutoka Tanzania, jumla ya wanajeshi 20 wa kulinda amani wameuawa mashariki mwa DRC tangu wiki jana wapiganaji wa M23 walipoingia Goma na kuanza makabiliano na jeshi la serikali.
Wanajeshi 14 kati ya 20 wanatoka Afrika Kusini na walikuwa miongozi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) waliotumwa nchini humo mwishoni mwa mwaka wa 2023.
Kikosi hicho kwa jina SAMIDRC pia kinashirikisha wanajeshi kutoka nchi zingine wanachama wa jumuiya SADC.
Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN) zaidi ya watu 700 wamekufa na wengine 2,800 kujeruhiwa ndani ya muda wa siku tano tano tangu mapigano yalipozuka mashariki mwa DRC.
Maelfu ya watu wametoroka makwao, wengi wakitorokea nchi jirani ya Rwanda. Baadhi ya waliotorokea nchi jirani ni wafanyakazi wa UN na Benki ya Dunia.
Wizara ya Afya nchini DRC inasema hifadhi za maiti zimejaa sawa na hospitali kiasi za kushindwa kuwahudumia waliojeruhiwa.
Duru zinasema kuwa baadhi ya miili ya watu waliouawa imetapakaa kwenye barabara za miji kutokana na msongamano kwenye hifadhi za maiti
Licha ya kuuawa kwa wanajeshi wake wawili, TPDF imetoa hakikisho kwamba wanajeshi wake waliosalia DRC wakihudumu chini ya kikosi Cha SAMIDRC “wako salama na wanaendelea na majukumu yao ya kulinda amani.”
Leave a Reply