Bungei asema polisi hawakuua Rex Masai wala vijana wengine wakati wa maandamano – Taifa Leo


MKURUGENZI wa masuala ya utoaji huduma katika makao makuu ya Polisi (NPS) Adamson Bungei aliambia mahakama ya Milimani kwamba polisi hawakuhusika na mauaji ya Rex Masai na wengine wakati wa maandamano ya Gen-Z kupinga maongozi ya serikali na Mswada wa Fedha mnamo Juni 20, 2024.

Bw Bungei aliyekuwa akitoa ushahidi katika uchunguzi wa kubaini kilichosababisha kifo cha Rex Masai alimweleza hakimu mkazi Geoffrey Onsarigo kwamba “polisi hawakuhusika na mauaji ya waandamanaji.”

Afisa huyo mkuu wa polisi alikana aliwaamuru maafisa wa polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wanapinga maongozi ya serikali ya Rais William Ruto.

Na wakati huo huo mahakama ilielezwa hakukuwa na maagizo ya kuzima maandamano mnamo Juni 20, 2024 kati kati mwa jiji la Nairobi.

“Hakuna afisa wa polisi alihusika na mauaji ya Rex Masai,” Bw Bungei alieleza hakimu alipoongozwa kutoa ushahidi na wakili wa serikali Gikui Gichuhi.

Afisa huyo wa polisi aliambia mahakama kwamba polisi walijulishwa baadaye kwamba Masai alipigwa risasi na kufia katika hospitali baada ya kupata jeraha mguuni.

“Baada ya mwili wa Rex Masai kufanyiwa upasuaji ilibainika kilichopelekea kifo chake ni jeraha la risasi,” Bw Bungei alieleza mahakama.

Kisa hicho kilipotendeka Bw Bungei alikuwa Kamanda wa Polisi eneo la Nairobi.

“Mnamo Juni mwaka jana kulikuwa na maandamano kati kati mwa jiji la Nairobi kuanzia saa mbili asubuhi.

Habari zilisambaa katika mitandao ya kijamii huenda kukawa na maandamano ya Gen-Z. Maandamano makuu yaliyosababisha uharibifu wa mali na utovu wa nidhamu kisha polisi waliingilia kuzima vurumai,” Bw Bungei alimweleza hakimu.

Akitoa ushahidi mbele ya Bw Onsarigo, Bw Bungei alisema ijapokuwa kulikuwa na maandamano polisi hawakumuua mwandamanaji huyu – Rex Masai.

“Kama Kamanda wa Nairobi nilihakikisha kuna doria za polisi kudumisha amani. Mnamo Juni 20, 2024 niliamuru polisi watulize ghasia. Sikujulishwa kuhusu mauaji mengine yoyote mnamo Juni 20, 2024. Nathibitishia hii mahakama kwamba polisi huwajibika mambo yakitokota. Vurugu au vuruami ikichipuka polisi hupelekwa kuzituliza,” Bw Bungei aliambia mahakama.

Kamanda wa Polisi eneo la Nairobi Bi Doris Mugambi alieleza mahakama pia alihusika katika mipango ya kuhakikisha kuna utulivu wakati wa maandamano ya Juni 2024.

Alisema polisi walipashwa habari kutakuwa na maandamano kisha wakajiandaa kukabiliana na waandamanaji kuhakikisha amani imedumishwa.

Alikariri kama Bw Bungei kwamba polisi hawakuhusika na mauaji ya Rex Masai.

Video za maandamano zilichezwa mahakamani huku polisi wakionekana wakiwapiga risasi Gen-Z waliokuwa wamejihami kwa vitambaa na chupa za maji.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*