SHUGHULI za masomo zilisitishwa Jumatano, Februari 5, 2025 katika shule kadhaa Kaunti ya Uasin Gishu baada ya walimu kususia kazi na kuvamia afisi za kampuni za bima ya Aon-Minet na kituo cha kiafya cha Bliss Medical Centre wakilalamikia huduma mbovu.
Walimu hao wenye hasira walivamia afisi za AoN-Minet katika jumba la Daima Tower jijini humo na kumtoa meneja wa kanda, wakamwingiza kwa gari na kumpeleka hadi Bliss Medical Centre katika jumba la Zion Mall wakitaka kampuni hiyo ya bima iwaruhusu kusaka huduma katika hospitali wanayotaka.
Wakiongozwa na Katibu wa chama cha walimu wa shule za upili (KUPPET) tawi la Uasin Gishu Elijah Maiyo walisema kuwa hatua ya kampuni hiyo ya bima kuwalazimu kusaka huduma kutoka hospitali fulani imewaletea wengi wao shida.
Bw Maiyo aliikosoa hatua ya kampuni hiyo kusitisha huduma katika hospitali mbalimbali na kuwalazimisha kusaka huduma katika hospitali walizozitaja kama mbovu.
“Wanachama wetu wanaougua kisukari na magonjwa mengine sugu hawawezi kupata huduma kutoka kwa madaktari wanaowazoea kutokana na maagizo ya kiholela kutoka kwa kampuni yetu ya bima, inayotulazimu kutafuta huduma katika hospitali za viwango vya chini, vinavyohudumu kama vioski,” akalalama Bw Maiyo.
Walimu hao wenye ghadhabu wameipa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kuingilia kati suala.
Walimu wa kike walidai kuwa hospitali zinazopendekezwa na kampuni hiyo ya bima huwa hazitoi huduma bora kwa wale waja wazito.
“Walimu wa kike wanalazimishwa kujifungua katika mazingira mbovu katika baadhi ya hospitali hizi zenye msongamano kiasi kwamba baada ya akina mama wanalazimika kujifungua ndani ya vyoo vya hospitali hizo,” akadai Celestine Cheptolo, mwakilishi wa jinsia katika Kuppet.
Kufuatia malalamishi yaliyoibuliwa na walimu, Katibu Mkuu wa chama cha kitaifa cha walimu nchini (Knut) Collins Oyuu amechukua hatua ya haraka na kuamuru kampuni ya AoN-Minet iwaruhusu walimu kutafuta huduma kutoka hospitali wanazopendelea.
Akiongea katika mkahawa wa Eka jijini Eldoret Jumatano, Bw Oyuu alitisha kuwa walimu wataiolazimisha TSC isitishe kandarasi yake na kampuni hiyo ya bima ikiwa matakwa yao hayatatimizwa.
“Sharti TSC iingilie kati changamoto hii wa kwa sababu ilipeleka pesa zetu kwa AoN-Minet. Tunaiambia TSC kwamba iwapo mambo hayatarekebishwa kutatoa msimamo wetu ili walimu wapate huduma kwa pesa wanazolipa,” akasema Bw Oyuu.
Aliandamana na Makatibu wa Knut kutoka kutoka ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa wakiwemo Sammy Bor (Uasin Gishu) Martin Sembelo (Pokot Magharibi) na Josephat Serem kutoka Nandi miongoni mwa maafisa wengine wa chama hicho.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA
Leave a Reply