![dnIMAGESdemo3012f-1320x792.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/dnIMAGESdemo3012f-1320x792-678x381.jpg)
MAHAKAMA Kuu imebatilisha uamuzi wa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja wa kupiga marufuku maandamano ya kuipinga serikali katikati ya jiji la Nairobi na kuwataka waandamanaji kuteua kiongozi.
Jaji Bahati Mwamuye jana alisema taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na polisi Julai 17, 2024 ikipiga marufuku maandamano ya umma ilikuwa ni kikwazo kwa haki za binadamu na hivyo basi ni kinyume cha katiba.
Inspekta jenerali alitangaza marufuku hiyo, akisema maandamano yaliyoongozwa na vijana, ambayo yalizuka Juni 2024, yaliingiliwa na magenge ya wahalifu na kwamba kukosa kuwa na kiongozi kulifanya iwe vigumu kwa polisi kutekeleza mpango wa usalama.
Bw Kanja alitaja ripoti za kijasusi ambazo alisema zilionyesha kuwa magenge ya wahalifu yaliyopangwa yalikuwa yakitumia vibaya maandamano hayo ili kutekeleza uhalifu ikiwemo kupora maduka.
“Kwa kuzingatia jukumu letu la Kikatiba na kwa maslahi ya usalama wa taifa, tunapenda kufahamisha umma kwamba tuna taarifa za kijasusi za kuaminika kwamba magenge ya wahalifu yaliyopangwa yanapanga kutumia maandamano yanayoendelea kushambulia watu ikiwa ni pamoja na uporaji,” alisema.
Lakini ikikubali ombi la shirika la Katiba Institute, mahakama ilisema hakuna hitaji kwamba maandamano lazima yawe na kiongozi aliyeteuliwa kushirikiana na polisi.
“Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Inspekta Jenerali ilikuwa kinyume na katiba kiasi kwamba iliweka sharti la lazima kwamba ili kufurahia haki ya kuandamana, lazima kuwe na kiongozi aliyeteuliwa ambaye anapaswa kushirikiana na polisi wakati wa maandamano”.
Katika ombi lake, Katiba Institute ilipinga uamuzi wa Inspekta Jenerali wa kupiga marufuku maandamano kwa muda usiojulikana.
Leave a Reply