![trump-amerika-1320x792.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/trump-amerika-1320x792-678x381.jpg)
TANGU aapishwe na kutwaa madaraka mnamo Januari 20, Rais wa Amerika Donald Trump ametetemesha ulimwengu sera zake zikisababisha kilio na kuvutia ghadhabu za nchi kadhaa.
Kenya ni kati ya mataifa ambayo sera hasi za Rais Trump zimeanza kuwaathiri wengi mamia wakianza kupoteza kazi kufutia kuondolewa kwa ufadhili wa Amerika.
Tukio la hivi punde la Rais Trump ambalo limezua ghadhabu miongoni mwa nchi za Kiarabu ni tangazo lake kuwa atawaondoa Wapalestina kwenye ukanda wa Gaza.
Akizungumza baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Jumatano, Rais Trump alisema kuwa atawaondoa Wapalestina Gaza kisha astawishe eneo hilo liwe kama nuru ya ukanda wa Mashariki ya Kati.
Kwake hii ni kati ya mikakati ambayo itahakikisha kuwa vita vya miaka mingi kati ya Israel na Hamas, vinapata utatuzi wa milele.
“Amerika itachukua usimamizi wa ukanda wa Gaza, ijenge upya ukanda huo, iumiliki na kuugeuza kituo kikubwa cha kitalii pamoja na kitovu cha ajira, Gaza itakuwa mwanga na nyota ya Mashariki ya Kati,” akasema Rais Trump.
Hatua yake hiyo imeungwa mkono na Israel huku akipendekeza raia wa Gaza waende waishi Misri na Jordan. Hata hivyo, mataifa yenye uchumi mkubwa ya kiarabu kama Iran na Saudi Arabia pamoja na yale ya Ulaya (EU) kama Urusi, Uhispania, Ujerumani kisha Uingereza yamepinga mpango huo wa Rais Trump.
Hamas wenyewe wamesema kuwa katu hawataondoka kwenye ardhi yao na kauli ya Rais Trump inakuja wakati mazungumzo yamekuwa yakiendelea ya kupatanisha kundi hilo na Israel. Kauli yake iwapo itatekelezwa inahofiwa itazua vita ulimwenguni.
Baada tu ya kutwaa mamlaka, Rais Trump alianzisha mchakato wa kuondoa Amerika kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO) akitoa notisi ya mwaka mmoja ulioashiria kuwa hawatakuwa sehemu ya shirika 2026.
Amerika ndiyo mfadhili mkubwa wa shughuli za WHO ambapo ilitumia jumla ya Sh165 bilioni mwaka jana na huchangia asilimia 18 ya ufadhili wake.
Rais Trump alisema shirika hilo limekuwa likinyonya Amerika ambapo kila mwaka hutumia zaidi ya Sh65 bilioni akidai shughuli za WHO hazinufaishi raia wake.
Alilinganisha mchango wa Amerika na China ambayo hutoa Sh5 bilioni pekee ilhali ina watu zaidi ya bilioni 1.4 huku Amerika ambayo ina watu milioni 341 ikitoa hela nyingi.
“Hakuna haki katika hilo,” akasema Rais Trump. Kutokana na umuhimu wa Amerika kwenye WHO ambayo ina mataifa wanachama karibu 200, shirika hilo lilitoa taarifa na kurai Rais Trump awazie upya uamuzi wake.
WHO imekuwa ikishughulika na miradi mbalimbali ya kiafya kama sehemu ya kupambana na magonjwa sugu yanayotatiza mataifa mbalimbali. Kwa zaidi ya miaka 70, WHO imekuwa ikishirikiana na USA kupambana na tetekuwanga (chicken pox, malaria, Ukimwi na kifuakikuu.
“Lazima tuingiwe na wasiwasi kwa sababu serikali zetu zimekuwa zikitegemea ufadhili wa kigeni kupambana na Ukimwi. Kenya sasa itapata wapi Sh40 bilioni za kupambana na Ukimwi?” akasema Dkt Gitahi Githinji ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Amref Health Afrika akirejelea athari ya Amerika kujindoa WHO kwa Kenya.
Rais Trump ameweka wazi kuwa Amerika inaweza kufadhili tu WHO iwapo itasimamiwa na kudhibitiwa na serikali yake.
Amependekeza hata Afisa Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aondolewe na wadhifa huo upewe raia wa Amerika.
Maelfu nao wanakodolewa macho na kupoteza ajira baada ya Wafanyakazi katika Shirika la USAID kutumwa kwenye likizo ya lazima kuanzia leo (Februari 7) baada ya barua kutumwa Jumatano.
Ulimwenguni, wafanyakazi wa USAID ni zaidi ya 10,000 na kuna kazi nyingine za chini ambazo zimeajiri maelfu na kuwasaidia kukimu familia zao.
Waziri wa Masuala ya Nje wa Amerika Marco Rubio Jumatano alisema shirika hilo halijakuwa likitekeleza majukumu yake vyema na wafanyakazi wake hawawezi kuyajibu hata maswali ya kimsingi kuhusu mipango yake.
Utawala wa Trump umeweka wazi kuwa utaigeuza USAID kuwa sehemu ya idara ya serikali ili kufuatilia utendakazi wake na kuidhibiti. Bilionea Elon Musk hata alidai shirika hilo hutumia fedha za Amerika kufadhili ugaidi.
Rais Trump tayari ameanzisha vita vya kibiashara dhidi ya China ambapo wiki hii alitishia kuongeza ushuru wa asilimia 10 kwenye bidhaa zake zinazoingizwa Amerika.
Hata hivyo, China ilijibu kwa kuongeza ushuru wa asilimia 15 kwenye gesi ya Amerika huku utawala wa Rais Trump ukiweka asilimia 10 ya ushuru kwenye mafuta ghafi, pembejeo za kilimo, malori, injini kubwa za magari kutoka China.
Ubabe wa kutekeleza ushuru huo usipotatuliwa, basi utaanza kutekelezwa mnamo Jumatatu. China tayari imelalamikia Shirika la Kibiashara Ulimwenguni (WHO) ikilaumu Amerika kwa kuvunja sheria za kimataifa za kuendesha biashara.
Urusi ilikuwa na matarajio mengi kuwa Rais Trump ataegemea upande wao kwenye vita dhidi ya Ukraine.
Hata hivyo, Rais Vladimir Putin amejipata pabaya baada ya Rais Trump kutishia kuongeza ushuru na vikwazo vya kiuchumi iwapo Urusi haitalegeza kamba na kukomesha vita dhidi ya Ukraine.
“Bila maelewano, sitakuwa na budi ila kuweka ushuru wa juu na vikwazo katika kila bidhaa ambazo Urusi inauzia Amerika pamoja na mataifa mengine,” akasema Rais Trump mnamo Januari 22 akisema vita hivyo lazima vitamatike ndani ya siku 100 kutoka Januari 20.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ni kiongozi wa kwanza Afrika kuonja makali ya Rais Trump aliyedai kuwa sera zake za umiliki wa ardhi zinabagua watu weupe na Amerika itakomesha ufadhili kwa nchi hiyo.
Leave a Reply