Sina haraka na miungano, bora Ruto asipate muhula wa pili – Taifa Leo


KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka atalazimika kusubiri kauli za kisiasa zitakazotolewa na kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua wiki chache zijazo kabla ya kuamua kuunda muungano mpya wa kumuondoa mamlakani Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, Bw Musyoka ameweka wazi kuwa yeye ndiye mgombeaji bora zaidi kukabiliana na Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais kwani anayo tajriba tosha.

“Aidha, nimeonyesha kuwa ninaweza kuwaachia wengine kwa manufaa ya taifa hili na kwamba ninaweza kufanya kazi na viongozi katika vyama vyote vya kisiasa,” Bw Musyoka akasema.

Bw Musyoka alisema hayo jana asubuhi kwenye mahojiano katika vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo kwa Kiluhya alipoangazia masuala mengine kama vile uchumi, ufisadi, afya, na mzozo katika taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Bw Musyoka pia alizungumzia sera mpya za Rais wa Amerika Donald Trump na jinsi zinavyoathiri Kenya.

Bw Musyoka alifanya mahojiano katika idhaa hizo siku mbili tu baada ya Bw Gachagua kufanya hivyo, ambapo alimkosoa Rais Ruto na kuwataka watu wa Jamii ya Mulembe kujiunga na muungano mpya unaoundwa kumzuia Ruto kuhudumu muhula wa pili kama rais.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema maamuzi yatakayofanywa na Bw Gachagua na Raila au vyama vyao, yatakachangia pakubwa katika kuundwa kwa muungano huo.

Uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) unafanyika Februari 15 na 16, ambapo Bw Odinga anamenyana na wagombeaji wengine wawili.

“Raila anawania wadhifa wa AUC na tunamtakia ushindi kwani ushindi wake ndio utakuwa furaha yetu. Tunasubiri matokeo ya uchaguzi huo kubaini ikiwa, bila kujali matokeo yake, ODM itatuunga mkono katika ajenda hii ya kumwangusha Ruto.

“Hatutegemei Raila kama Azimio katika kuendelea na mipango yetu, ila tunataka muungano utakaoshirikisha watu wote, wakiwamo wafuasi wa ODM,” akasema Bw Musyoka.

Endapo Bw Odinga atashinda, Dkt Ruto anatarajia kurithi ngome zake kwani usaidizi aliopata kutoka serikali utakuwa umezaa matunda.

Lakini baadhi ya wakosoaji wa Dkt Ruto wanaamini kuwa endapo kiongozi huyo wa ODM atashindwa, Bw Odinga atajiunga na muungano mpya unaolenga kuungana na wananchi kumzuia Ruto kusalia Ikulu kwa muhula wa pili.

Wakati wa mahojiano hayo ya saa moja unusu, Bw Musyoka alishikilia kuwa hajaanzisha ushirikiano wowote na Bw Gachagua.

Hata hivyo, alieleza kuwa atasubiri tangazo la kisiasa ambalo mbunge huyo wa zamani wa Mathira, Nyeri atatoa Jumapili kabla ya kuamua ikiwa atashirikiana naye au la.

Bw Musyoka alisema chama cha Wiper hakikuunga mkono hoja ya kumwondoa afisini Bw Gachagua kwa sababu kilitaka aondolewe pamoja na Rais Ruto.

Hii kulingana naye, ndiyo imefanya wafuasi wa Bw Gachagua kumshabikia kwa wingi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*