Trump awaendea wafanyakazi wa ICC wanaochunguza Amerika – Taifa Leo


 

WASHINGTON, AMERIKA

RAIS Donald Trump jana alifikia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) akiweka vikwazo vya usafiri na kiuchumi kwa wafanyakazi wa korti hiyo ambao wanachunguza  kesi zinazolenga Amerika, raia wake au washirika wake kama Israel.

Kiongozi huyo amerudia marufuku ambayo aliiwekea ICC  katika muhula wake wa kwanza kati ya 2016-2020.

Mnamo Ijumaa (jana) ICC ilishutumu hatua hiyo na kuwataka mataifa 125 wanachama wake  waunge mkono wafanyakazi wake wanaolengwa na Amerika.

“Mahakama inasimama wima na wafanyakazi wake na inaahidi kuendelea kupigania haki na matumaini kwa mamilioni ambao wamedhulumiwa kote ulimwenguni tena katika hali zote,” ikasema taarifa ya ICC.

Kauli ya Rais Trump imetokea baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutembelea Washington na kukutana naye Jumatano wiki hii.

Netanyahu pamoja na aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Israel na kiongozi mmoja wa Hamas, wanaandamwa na ICC kuhusiana na vita ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa Ukanda wa Gaza.

Vikwazo alivyoweka Rais Trump ni kutwaa mali ya wafanyakazi wa ICC iliyoko Amerika kisha kuwazuia pamoja na familia zao kutembelea nchi hiyo.

Uholanzi ambako ICC inapatikana, Ijumaa ilisikitishwa na uamuzi wa Rais Trump.

“Mahakama inapambana tu na ukiukaji wa haki za kibinadamu,” akasema Waziri wa Masuala ya Kigeni Casper Veldkamp.

Wakati wa muhula wake wa kwanza, Rais Trump aliweka vikwazo kwa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Mashtaka wa ICC Fatou Bensouda pamoja na mmoja wasaidizi wake wakuu.

Alifanya hivyo baada ya ICC kuanza uchunguzi kwenye uhalifu wa kivita ambao  wanajeshi wa Amerika walidaiwa kutekeleza wakidumisha amani Afghanistan.

Hatua ya Rais Trump imeanza kuchemsha ulimwengu Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, mshirika wake kiongozi huyo, akisema nao wanatathmini kuondoka ICC.

“Wakati umefika Hungary itathmini inafanya nini ICC ambayo imewekewa vikwazo na Amerika. Kweli wimbi la Trump linatikisa ulimwengu,” akasema Orban

Amerika, Israel, China na Urusi ni baadhi ya mataifa makubwa ambayo si wanachama wa ICC.

Hata hivyo, mahakama hiyo ina sheria ambayo inairuhusu kuwahukumu viongozi ambao wanaendeleza dhuluma dhidi ya wanachama wake.

Ili kupungaza makali ya athari za kiuchumi kutokana na vikwazo vya Amerika, ICC wiki hii iliwalipa wafanyakazi wake mshahara wa miezi mitatu.

Kando na Amerika, Urusi pia imewekea ICC vikwazo baada ya hati kutolewa ya kukamatwa kwa rais wake Vladimir Putin miaka Machi 17, 2023. Rais Putin anadaiwa kutekeleza uhalifu wa kivita wakati ambapo nchi hiyo imekuwa ikikabiliana na Ukraine.

Urusi inawaandama Kiongozi wa Mashtaka wa ICC Karim Khan pamoja na majaji wawili wa mahakama hiyo, ikiwalaumu kwa kulenga taifa hilo visivyo.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*