MSHINDI wa nishani ya fedha mbio za mita 10,000 katika mashindano ya Riadha za Dunia, Daniel Simiu, ataongoza orodha ya watamkaji matata kwenye Mbio za Nyika za Kitaifa jijini Eldoret mnamo Jumamosi zinazodhaminiwa na kampuni ya Betika.
Simiu, ambaye alijitosa katika mbio za mita 42 akimaliza Chicago Marathon katika nafasi ya tano mwaka 2024, atalenga kudhihirisha ubabe wake anapojiandaa kwa msimu wa mbio za uwanjani utakaoanza wikendi ijayo.
Mtimkaji huyo anayefanyia mazoezi eneo la Iten katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, alitawala mbio za nyika za Bomet mwezi Desemba 2024. Alitangaza mjini Bomet kwamba bado hajaacha mbio za uwanjani.
Ataingia mbio za kitaifa na motisha baada ya kunyakua ushindi kwenye Mbio za Nyika za Idara ya Polisi hapo Januari 17.
Simiu alikosa Michezo ya Olimpiki 2024 baada ya kujikwaa na kuanguka wakati wa kuchaguliwa kwa timu ya taifa ya 10,000m kwenye duru ya Eugene Diamond League nchini Amerika ambayo alimaliza katika nafasi ya nane kwa dakika 27:24.33. Daniel Mateiko alishinda mjini Eugene kwa kuandikisha dakika 26:50.81.
“Bado sijastaafu mbio za uwanjani na baada ya kumaliza Chicago Marathon katika nafasi ya tano, nimeamua kumakinika katika mbio za nyika kabla ya kubadilisha gia kuanza matayarisho ya Riadha za Dunia zitakazoandaliwa mjini Tokyo, Japan baadaye mwaka huu ambapo nalenga kupata tiketi ya 10,000m,” Simiu alisema katika mahojiano ya awali.
Atapimwa vilivyo weledi wake na bingwa mara tano wa jeshi la KDF, Kibiwott Kandie anayemezea mate taji.
Baada ya kushinda mbio za nyika za majeshi kwa mara ya tano mwezi Januari, Kandie alitangaza kuwa ataelekeza nguvu zake kwa mbio za barabarani, akilenga kuimarisha matokeo yake katika marathon.
Kandie atashirikiana na Simon Koech, Peter Ruto, Abel Mutai na Hillary Kipkoech kutoka jeshi.
Mbali na Simiu na Kandie, macho pia yatakuwa kwa bingwa mpya wa mbio za nyika za Discover Kenya, Cornelius Kemboi ambaye anatumai kushiriki Riadha za Dunia mjini Tokyo mwezi Septemba.
“Nitashiriki pia mbio za nyika za kimataifa za Sirikwa wiki mbili zijazo,” akasema Kemboi na kufichua kuwa atamakinikia mbio za 5,000m uwanjani.
Katika kitengo cha wanawake, bingwa wa mbio za 10km za Idara ya Polisi, Sheila Chelangat amebashiri kutakuwa na ushindani mkali akiamini kuwa kila mtimkaji amejiandaa vilivyo.
Baadhi ya washindani wake wakuu ni pamoja na mshindi wa medali ya shaba ya Nusu-Marathon Duniani Catherine Reline, Christine Njoki, Maureen Jepkoech na Monica Chebet kutoka kutoka North Rift.
Mashabiki pia watapata kuona bingwa wa zamani wa London Marathon Joyciline Jepkosgei kutoka KDF anayepanga kushiriki London Marathon nchini Uingereza mwezi Aprili.
Kuna tuzo ya Sh200,000, Sh130,000, Sh100,000, Sh70,000, Sh50,000, Sh40,000, Sh30,000, Sh20,000 na Sh10,000 kwa 10-bora katika mbio za 10km, mtawalia.
Tuzo ya chipukizi, ambao ni washiriki wenye umri wa miaka 20 ama chini, ni Sh140,000, Sh90,000 na Sh70,000 kwa tatu-bora, huku nambari tatu za kwanza katika mzunguko wa 2km zikiandamana na zawadi na Sh50,000, Sh40,000 na Sh30,000, mtawalia.
Leave a Reply