![ruto-isiolo-ijumaa.jpeg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/ruto-isiolo-ijumaa-678x381.jpeg)
ZAIDI ya watu 40 Jumapili walikamatwa mjini Isiolo kwenye oparesheni ambayo ililenga wauzaji wa mihadarati, pombe haramu na wale waliopatikana wakizurura ovyo ovyo baada ya saa sita usiku.
Kamishina wa Kaunti Geoffery Omoding Jumapili aliambia Taifa Leo kuwa oparesheni hiyo ni kutokana na ahadi ya Rais William Ruto mnamo Ijumaa kuwa serikali itawakabili wale ambao wanasafirisha dawa za kulevya Isiolo na Marsabit.
Hata hivyo, kumeibuka madai kuwa oparesheni hiyo iliendelezwa kuwakabili wale ambao walimzomea Rais Ruto, Gavana Abdi Guyo na Seneta Fatuma Dullo.
Hata hivyo, Bw Omoding alipuuza kuwa kamatakamata hizo zilitokana na kuzomewa kwa Rais na wanasiasa hao. Makundi ya vijana yalishindana kuwazomea viongozi baada ya Rais kuzindua Mradi wa ujenzi wa kujenga kiwanda cha kisasa Isiolo.
“Vijana ambao walikuwa wakiwazomea viongozi walitia kaunti hii aibu kutokana na tofauti za kisiasa kati ya gavana na seneta. Kuna suala la mihadarati ambalo ni tofouti na watu 43 waliokamatwa, watafikishwa kortini baada ya uchunguzi kukamilika,” akasema Bw Omoding.
“Kuna kundi dogo ambalo lilikuwa likimzomea rais na lilifanya hivyo baada ya mshukiwa mkuu wa kulangua mihadarati kunyakwa wiki jana. Amekuwa akitumia mchezo wa soka kuuza mihadarati kwa vijana,” akasema Bw Omoding.
Kamishina huyo alisema kuwa ulanguzi wa dawa za kulevya umefikia kiwango hatari Isiolo kiasi kuwa washukiwa sasa walikuwa wakiwapa hongo maafisa wa usalama.
“Walanguzi wa dawa hizo wanatoka Shashamane Ethiopia na maeneo ya mashinani Marsabit na Isiolo. Hapo nyuma tuliwakamata washukiwa lakini wakipelekwa Nairobi wanawaachiliwa kwa njia ya kutatanisha,” akaongeza.
Mnamo Ijumaa Rais aliamrisha oparesheni ya kuwakamata walanguzi wa dawa za kulevya Isiolo na Marsabit akisema imesababisha tabia hiyo ienee hadi kaunti jirani.
Huku vijana hao wakizomeana, Rais Ruto alisema baadhi yao walikuwa wametumwa na walanguzi wapige kelele katika mkutano wake.
“Nimejua mmetumwa lakini nawaonya hamwezi kutishia serikali yangu. Raia wa kigeni hawezi kuja na kugeuza Isiolo danguro la dawa za kulevya. Haitafanyika,” akasema Rais Ruto.
Leave a Reply