Wafanyakazi wa mjengo waripoti pato zuri, biashara za rejareja zikilia hali ngumu – Taifa Leo


WAFANYAKAZI katika sekta ya ujenzi wameripoti ongezeko la juu zaidi la mishahara katika utafiti mpya wakati ambao mapato ya Wakenya wengi hasa wanaolipwa mshahara kila mwezi yakipungua.

Watu wengi kulingana na utafiti waliripoti kushuhudia ongezeko la mapato hasa kuhusiana na mali isiyohamishika, ambayo inajumuisha majengo na ujenzi.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 22 waliripoti kuongezeka kwa mapato katika sekta hii ikilinganishwa na asilimia 14 katika viwanda na biashara na asilimia 13 katika uuzaji wa jumla na rejareja.

Hata hivyo, kati ya sekta tano zilizochambuliwa katika matokeo ya utafiti wa kampuni ya ICEA LION Asset Management, uuzaji wa jumla na rejareja ulikuwa na watu wengi zaidi ikiwa ni asilimia 33 ambao waliripoti kupungua kwa mapato.

Sekta ya hoteli, utalii na burudani ilikuwa na watu wengi zaidi walioripoti kuwa mapato yao yamekwama bila kuongezeka au kushuka wakiwa ni asilimia 66.

Watafiti walihusisha hili na miradi mingi ya ujenzi inayoendelea kama vile mijengo, mabohari ya viwanda na nyumba za makazi ambayo mingi inatekekezwa na wawekezaji wa kigeni.

Judd Murigi, Mkuu wa Utafiti na Usimamizi wa Mali wa ICEA LION Asset Management, pia alihusisha mapato yaliyoimarika na miradi ya nyumba za bei nafuu kote nchini.

“Miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu pia inaweza kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya wafanyikazi wa ujenzi,” alisema.

Walioripoti kuongezeka kwa mapato pia waliripoti kuongezeka kwa matumizi.

“Ongezeko la juu zaidi la mapato ni kwa wafanyikazi katika sekta ya mali isiyohamishika na ujenzi, ambapo asilimia 86 ya waliohojiwa waliripoti ongezeko la matumizi,” utafiti unafichua.

Utafiti ulikusanya maoni kutoka kwa wafanyabiashara 233 wa rejareja na watu 1,210.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*