MAHAKAMA ya Machakos imesema maafisa wakuu wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Mavoko walidharau korti kwa kukosa kutekeleza agizo la mahakama na kusababisha ubomoaji wa majengo katika ardhi inayozozaniwa.
Wamiliki kadhaa wa nyumba wanaoishi katika ardhi inayozozaniwa L.R No 8784/1 iliyoko eneo la Daystar, waliwasilisha kesi kortini wakitaka mahakama iwaokoe wasitimuliwe.
Mnamo Januari 27 2025, Hakimu Mkuu Mwandamizi James Omburah alitoa amri ya muda ya kuzuia Kilimanjaro Construction Limited, Lalji Hirani, Chuo Kikuu cha Daystar na wengine katika kesi hiyo, wao wenyewe au maajenti wao kubomoa majengo ya walalamishi, kuchimba au kutekeleza shughuli zozote za ujenzi kwenye ardhi hiyo kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi.
Hata hivyo, kesi Nambari E066 ya 2025 iliyotajwa Februari 10, 2025, wakili wa walalamishi Bi Anita Mwende alifahamisha mahakama kuwa licha ya agizo la korti, OCS wa kituo cha polisi cha Athi River na OCPD wa eneo la Athi River Mashariki, ubomoaji ulifanyika mnamo Januari 28 2025 chini ya ulinzi wa polisi.
Zaidi ya hayo, wakili wa walalamishi alieleza mahakama kuwa hatua ya maafisa wa polisi ya kutotekeleza agizo la mahakama kulisababisha hasara kubwa kwa walalamishi ambao mali yao iliharibiwa.
Mshtakiwa wa pili (Lalji Hirani) kupitia kwa wakili wake aliomba kuwasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo huku wakili anayedaiwa kuwakilisha Chuo Kikuu cha Daystar akitaka kushirikishwa katika kesi hiyo.
Hakimu Omburah alisema maafisa wakuu wa polisi walidharau mahakama na wanaweza kuadhibiwa kwa kutofuata agizo la mahakama.
Aidha, aliongeza muda wa agizo la kuzuia washtakiwa kuendeleza ardhi hiyo hadi Machi 17 2025 kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Leave a Reply