NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki jana alisema yupo tayari kugharimika kisiasa iwapo hilo litachochewa na hatua yake ya kufanikisha miradi ya serikali eneo la Mlima Kenya.
Profesa Kindiki alisema hawezi kupoteza wakati wake kucheza siasa za ubabe ilhali kama naibu rais ana wajibu wa kumsaidia Rais William Ruto kutimiza ahadi walizotoa kwa Wakenya na wakazi wa eneo hilo wakati wa kampeni za 2022.
“Rais amesema mara nyingi kuwa iwapo kubadilisha nchi kutamgharimu umaarufu, basi yuko tayari. Hata mimi nasema kama msaidizi wake kuwa kama kuwahudumia Wakenya kutatugharimu umaarufu wetu, basi na iwe hivyo, niko tayari,” akasema Profesa Kindiki.
Naibu Rais alisema si muda ambao kiongozi huwa mamlakani ndio huwa na maana ila miradi ambayo wanatekeleza wakati ambapo wapo uongozini hata kama ni kwa kipindi kifupi.
“Kuna watu wamekazana eti muhula moja na nawaambia hilo si lolote kwetu. Watu wasitutishe eti tunahudumu muhula moja, sisi tunaangazia maendeleo na wakati mwingine kutekeleza hayo mambo, lazima uchungu uhisiwe,” akaongeza.
Alikuwa akiongea katika makazi ya naibu rais mtaani Karen alipokutana na viongozi wa Kaunti ya Kiambu kuweka mikakati ya kukamilisha miradi ya maendeleo.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amenukuliwa mara kadhaa akisema kuwa atahakikisha kuwa Rais Ruto anahudumu muhula moja pekee. Hata hivyo, Profesa Kindiki alisema yeye pamoja na Kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah hawatetereka kutokana na mawimbi ya kisiasa ya Bw Gachagua ila watamanikia majukumu yao.
“Kimani Ichung’wa kwa wakati mwingine utahisi umaarufu umeenda lakini jipe moyo na uendelee kufanya kazi kwa Wakenya. Wewe ndio msukuma ajenda za serikali bungeni na wale wanaoongea kwa kiburi wajue hakuna mtu anawamiliki raia wala kumuumba mtu,” akasema Profesa Kindiki.
Hata hivyo, alisema wapo tayari kuvurugana na wanaongea kwa kiburi na ifikapo mnamo 2027, Bw Gachagua na kundi lake watashangaa debeni.
“Ni ajenda gani ya Kiambu ulisukuma mbele ulipokuwa uongozini?. Hata Kalonzo naye pia amewahi kuwa makamu wa rais, watuambie waliwafanyia Wakenya nini kwanza,” akasema.
Leave a Reply