Msisherehekee mapema ushindi wa Raila huko AUC, Mukhisa Kituyi aonya – Taifa Leo


ALIKUWA Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) Mukhisa Kituyi amewaonya wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani Rais Odinga dhidi ya kuwa matumaini makubwa kwamba atashinda kwa urahisi wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Bw Kituyi Jumatatu, Februari 10, 2025 alisema kuwa kampeni kali ambayo Bw Odinga amefanya katika mataifa mengi ya Afrika huenda isimsaidie kushinda kiti hicho kwani kuna masuala mengi ambayo huzingatiwa katika uchaguzi kama huo.

“Kwa mfano ilivyodhihirika katika chaguzi zilizopita mataifa yanayozunguza Kifaransa na yale ya Kiarabu hupiga kura pamoja. Kwa mfano, imekuwa vigumu kwa mataifa yanayozumzo Kifaransa kumpigia kura mgombeaji kutoka nchi isiyozungumza lugha hiyo,” akasema wakati wa mahojiano katika kipindi cha “Fixing The Nation” kwenye runinga ya NTV.

“Vivyo, hivyo, itakuwa vigumu kwa marais wa mataifa ya Kiarabu kumpigia kura mgombeaji asiyetoka mataifa hayo,” akaongeza Dkt Kituyi aliyehudumu kama Katibu Mkuu wa UNCTAD kwa miaka minane.

Alielezea wasiwasi kwamba huenda Bw Odinga, akawa na kibarua kikubwa kumshinda Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mohamuod Ali Youssouf “kwani lugha za Kifaransa na Kiarabu zinazungumzwa wingi Djibouti.”

Dkt Kituyi aliongeza kuwa hatua Rais William Ruto kuunga mkono Israel vita vilipolipuka katika Ukanda wa Gaza, Oktoba 2023 haikuchukuliwa vyema Afrika.

“Kwa sababu hiyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa mataifa ya Kiarabu yatapigia kura mgombeaji mwingine,” akaeleza.

Dkt Kituyi aliongeza kuwa hamna hakikisho kuwa Bw Odinga atazoa kura zote za kundi la mataifa ambako Kiingereza huzungumzwa kwa wingi (Anglophone) kwani huenda zingine zikamwendea mshindani wake kutoka Madagascar Richard Randriamandrato.

“Madagascar pia ni taifa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC), yenye jumla ya wanachama 16,” akaeleza.

Mabw Odinga, Youssouf na Randriamandrato wanalenga kujaza nafasi hiyo AUC kwani mshikilizi wa sasa Moussa Faki kutoka Chad anastaafu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.

Uchaguzi huo utafanyika Februari 15 na 16 wakati wa mkutano wa viongozi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Akiongea Jumatatu katika Bomas of Kenya, Bw Odinga alitangaza kuwa atakubali matokeo ya uchaguzi.

“Nikishinda itakuwa ushindi kwetu. Nikishindwa pia nitakubali matokeo,” akaelaza.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*