Hisia mseto Maraga akionekana kuchangamkia siasa – Taifa Leo


JAJI Mkuu Mstaafu David Maraga, ambaye tangu aondoke afisini 2021, amekuwa mtulivu ameonyesha dalili za kujitosa siasani kutokana na jumbe zake kwenye mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara anayofanya na makundi mbalimbali ya wananchi.

Aidha, baadhi ya Wakenya katika mitandao ya kijamii pia wamekuwa wakimhimiza kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais 2027.

Ikumbukwe kuwa kabla ya Desemba mwaka jana, Maraga alikuwa ametuma jumbe mara 13 pekee katika mtandao wa kijamii wa X tangu alipostaafu 2021.

Kimsingi, jumbe hizo zililenga kuzima habari feki na kutoa risala za rambirambi kufuatia vifo vya viongozi kadhaa mashuhuri wakiwemo rais wa zamani Mwai Kibaki na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Nchini Francis Ogolla.

Lakini kati ya Desemba 2023 na sasa Bw Maraga ametuma jumbe mitandaoni mara tisa, karibu sawa na alivyofanya ndani ya miaka minne iliyopita.

Jaji huyo Mkuu wa zamani alirejea kwa kishindo kupitia ujumbe wake wa Mwaka Mpya ambao pia uliishambulia serikali ya Rais William Ruto kufuatia ongezeko la visa vya Wakenya kutekwa nyara kwa namna ya kutatanisha. Ujumbe huo umesomwa na zaidi ya watu 30,000.

Mwezi mmoja baadaye mnamo Januari 31, 2024, Maraga alitoa taarifa nyingine akilaani utekaji nyara na mauaji ya kiholela.

“Hatuwezi kukimya. Maovu haya yanasaliti mustakabali wa taifa letu na hadhi ya Katiba yetu. Uongozi ambao unaruhusu mauaji na ukiukaji wa hali za kibinadamu unahatarisha uhalali wake.”

Tangu wakati huo, taarifa hiyo imefuatiliwa na zaidi ya watu 390,000.

Kando na kwenye mitandao ya kijamii, Bw Maraga pia ameonekana hadharani akifanya mikutano ya mashauriano na watu wa matabaka kadhaa.

Mnamo Februari 4, mwaka huu alikutana na kundi la wanaharakati wakiongozwa na Nyamisa Chelagat, waliomweleza kuhusu shughuli zake za kupigania utawala bora, utawala wa kisheria na uzingativu wa matakwa ya kikatiba.

Akithibitisha kuhusu mkutano huo alituma ujumbe mitandaoni kwamba: “Nilifurahishwa na kujitolea kwenu kuibadilisha Kenya kuwa mahala pazuri kwa wote. Juhudi za vijana za kupigania maisha bora nchini zinahitaji uungwaji mkono.”

Kisha mnamo Jumapili wiki jana, Bw Maraga — ambaye ni muumini wa Kanisa la Kiadventisti — alihudhuria ibada katika Kanisa la Kianglikana la ACK Holy Trinity eneo bunge la Kibra, Nairobi.

Hatua hii ishara kuwa analenga kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa kutoka hadhira pana.

“Katika harakati zangu za kufanya mazungumzo na vijana, walinialika katika Kanisa la ACK Holy Trinity katika mtaa wa Kibra, Nairobi kwa “Ibada ya Vijana” leo. Ibada iliongozwa na Kasisi wa kanisa hilo Barack Odour ambaye mahubiri yake yalihusu jinsi Musa aliwaongoza watoto wa Israel kutoka Misri. Baada ya ibada nilipata fursa ya kutangamana na baadhi ya vijana na nikafurahishwa na imani yake kuhusu Kenya mpya itakayoshughulikia masuala yanayowahusu.”

Kauli ya mwisho ya Bw Maraga imechochea makisio kwamba Jaji huyo Mkuu wa zamani analenga kujitosa katika ulingo wa siasa kwa kuwania kiti katika uchaguzi mkuu ujao.

Maraga aliandikisha historia kwa kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Baadaye, kwa ujasiri, alishauri kwamba Bunge la Kitaifa linafaa kufutiliwa mbali kwa kufeli kufikia hitaji la kikatiba kuhusu usawa wa kijinsia.

Sasa, baadhi ya watu wanajiuliza ikiwa yuko tayari kujitosa katika ulingo mchafu wa siasa ambao ni tofauti na ule wa kisiasa.

Hata hivyo, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wana tashwishi kuhusu uwezekano wake kufaulu katika ulingo huo alivyofanya mahakamani.

Kulingana na Bw Javas Bigambo wale wanaopigia debe Bw Maraga wanajidanganya kwamba anaweza kufaulu kwa misingi ya maamuzi makali aliyotoa mahakamani.

“Ikiwa Maraga anataka kuwania urais, je sifa kuu ni maadili pekee? Kwa misingi ya kuwavutia watu, yeye ni mdhaifu mno. Jumbe katika Facebook na X pekee haziwezi haziwezi kuvutia. Anafaa kufikia upya, kujipanga na kuondoa sifa ya zamani ya mwanasheria mtulivu na kuwa mwanasiasa mwenye maneno ya kuvutia,” Bigambo anasema.

Mwenzake Martin Andati ni mwepesi wa kupuuzilia mbali wazo kwamba Maraga anaweza kutetemesha ulinzo wa siasa, akataja umri wake mkubwa.

“Maraga ni mzee; alihudumu kama Jaji Mkuu. Alipostaafu alikuwa na umri wa miaka 70 au 72. Amejenga zaidi sifa zake kitaalum katika Idara ya Mahamama. Sidhani kama angetaka kuchafua hadhi yake kwa kujiingiza katika ulingo wa siasa,” anasema Andati.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*