Wetang’ula alivyotupa uamuzi wa mahakama katika jaa la taka – Taifa Leo


SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula Jumatano alionekana kukaidi agizo la mahakama kwa kutangaza mrengo wa Kenya Kwanza kuwa wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa.

Katika taarifa aliyosoma katika kikao na alasiri jana, Bw Wetang’ula aliamua kwamba Kenya Kwanza ina jumla ya wabunge 165 huku Azimio ikiwa na wabunge 154.

Alieleza kuwa idadi ya wabunge wa Kenya Kwanza imekadiriwa kwa kujumuisha wabunge 145 wa chama cha UDA, wabunge wanane wa chama cha Amani National Congress (ANC), wabunge sita wa Ford Kenya, wabunge wawili wa The Service Party (TSP) na mbunge mmoja kutoka kila moja ya vyama vya National Agenda Party of Kenya, Grand Dream Development Party, Democratic Party (DP) na Chama cha Mashinani (CCM).

Kwa upande wa Azimio, Bw Wetang’ula alieleza kuwa wabunge wake wanatoka vyama vya ODM (wabunge 83), Jubilee (28), Wiper (26), Kanu (6), Democratic Action Party (5), Kenya Union Party (3), United Party of Independence (2) na chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) inayowakilishwa na mbunge mmoja.

Spika alifafanua kuwa, jumla ya wabunge 14 kutoka vyama vya; United Democratic Movement (UDM), Pamoja African Alliance (PAA) Chama cha Mashinani (CCM) na Mandeleo Chap Chap (MCC) inayoongozwa na Waziri wa Leba Alfred Mutua hawako katika mrengo wa Kenya Kwanza wala Azimio.

Hii, kulingana na Bw Wetang’ula, vyama hivyo havijakamilisha “utaratibu wa kisheria wa kuondoka Azimio” baada ya kuwasilisha barua ya kutaka kujiondoa.

“Kwa hivyo, kwa msingi wa maelezo hayo na takwimu nilizotoa kuhusu idadi ya wabunge wa vyama katika kila mrengo, Kenya Kwanza ndio mrengo wa walio wengi na Azimio ni mrengo wa walio wachache. Uongozi wa Bunge unasalia ulivyokuwa zamani,” Bw Wetang’ula akatangaza.

Spika huyo alikariri kuwa majaji wa Mahakama Kuu, katika uamuzi wao wa Ijumaa wiki jana, hawakuamua kuwa Azimio ndio mrengo wa walio wengi.

“Katika uamuzi wao, jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu walibatilisha uamuzi wangu wa Oktoba 6, 2022 kwamba Kenya Kwanza ndio ulikuwa mrengo wa walio wengi. Hawakubaini ni mrengo upi ulio wa wengi na ule ambao ni wa wachache kwa sababu hawana mamlaka ya kufanya hivyo. Afisi ya Spika ndio yenye mamlaka ya kufanya uamuzi kuhusu suala hilo,” Bw Wetang’ula akaeleza.

Hata hivyo, katika uamuzi wao majaji Jairus Ngaa, John Chigiti na Lawrence Mugambi walisema Spika huyo hakuwasilisha ithibati kuwa Kenya Kwanza ndio ulikuwa mrengo wa wengi na “kwa hivyo amekiuka kipengele cha 108 cha Katiba”.

Katika uamuzi wake wa Oktoba 6, 2022, Wetang’ula alieleza kuwa baada ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022, vyama vitano tanzu vya Azimio vilitia saini mikataba ya ushirikiano na Kenya Kwanza na hivyo jumla ya wabunge 14 waliochaguliwa kwa tiketi za vyama hivyo “wanachukuliwa kama wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza.”

Vyama hivyo vilikuwa; MDG, UDM, PAA CCM na MCC.

Lakini jana, aligeuka na kusema kuwa wabunge 14 waliochaguliwa kwa tiketi za vyama hivyo, sio wanachama wa mrengo wowote ule.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*