Kundi lingine la waasi laua watu 51 nchini DRC wakiwemo watoto 18 – Taifa Leo


BUNIA, ITURI, DR CONGO

IDADI ya raia waliouawa na kundi lingine la wanamgambo linalofahamika kama CODECO Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imefika 51.

Hii inafuata shambulio lililotokea Jumatatu jioni dhidi ya mkusanyiko wa vijiji vya Djaiba katika jimbo la Ituri.

Wanamgambo hao waliteketeza nyumba zilizojaa raia, wakafyatua risasi na kuwakata vichwa wakazi katika vijiji hivyo huku wakiacha wengine na majeraha mbalimbali kwa mujibu wa chifu kijiji kimoja, wakili na mwanachama wa shirika la kutetea raia mnamo Jumanne.

Awali Jumapili usiku wanamgambo hao waliokuwa wamejihami kwa silaha kali walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani kabla kukabiliwa na Kikosi cha Walinda Usalama wa Umoja wa Mataifa Dr Congo (MONUSCO).

Wanajeshi wa MONUSCO mjini Goma katika koa wa North Kivu, DR Congo, mnamo Januari 25, 2025. PICHA | REUTERS

Mkuu wa vijiji hivyo vya Djaiba vinavyopatikana eneo la Djugu katika mkoa wa Ituri, Jean Vianney, alieleza kuwa wanamgambo hao wa CODECO walianza shambulio hilo mwendo wa saa mbili usiku Jumatatu na kuuawa takriban watu 52.

“Kuna watu wamejeruhiwa, wengi wameteketezwa katika nyumba zao,” alisema Vianney na kuongeza kuwa wanajeshi wa Congo na walinda usalama wa MONUSCO eneo hilo hawakuingilia kati.

Mbunge kutoka eneo la Djugu, Floribert Byaruhanga, alisema idadi aliyokukwa nayo ya watu waliofariki ni 51 wakati huo, wakiwemo watoto 18.

Nayo orodha ya mashirika ya kiraia Ituri ilionyesha kuwa watu 51 waliuawa usiku kucha kuanzia Jumatatu hadi Jumanne.

Aidha, mkazi wa Djaiba aliyenusurika mauaji hayo, Daniel Kisembo, aliambia Reuters kuwa alihesabu miili 51 mingi ilikuwa imeteketea.

Chimbuko la CODECO

CODECO ni mojawapo ya maelfu ya wanamgambo wanaopigania ardhi na rasilimali mashariki mwa Congo.
Wanamgambo wameshutumiwa siku za nyuma na Umoja wa Mataifa kwa mashambulio dhidi ya jamii nyingine ikiwa ni pamoja na wafugaji wa Hema ambayo yanaweza kujumuisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Msemaji wa Jeshi la Mkoa, Jules Ngono, alisema wanajeshi walijaribu kusaidia lakini walifika wakiwa wamechelewa.
Naye msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, Jean-Tobie Okala, alisema katika taarifa yake kwamba walinda amani wamefanikiwa kuwalinda watu waliokimbia makazi yao katika kambi hiyo.
“Hili ni jambo la kusikitisha mno raia kuuawa wakiwa kambini. Hata hivyo, walionusurika wako salama,” akasema Okala.

Waasi wa M23
Haya yanajiri huku duru za kisiasa na za kidiplomasia zikisema kwamba Afrika Kusini imetuma wanajeshi zaidi pamoja na zana za kijeshi Mashariki mwa Congo mwezi mmoja tu baada ya wanajeshi wake 14 kuuawa katika mapigano na waasi wa kundi la M23.
Haya yanafanyika huku kukiwa na wasiwasi kuwa huenda mapigano hayo yakasambaa na kuwa mabaya zaidi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*