![drc-wakimbizi-1320x792.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/drc-wakimbizi-1320x792-678x381.jpg)
BUNIA, ITURI, DR CONGO
IDADI ya raia waliouawa na kundi lingine la wanamgambo linalofahamika kama CODECO Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imefika 51.
Hii inafuata shambulio lililotokea Jumatatu jioni dhidi ya vijiji vya Djaiba katika eneo la Djugu mkoa wa Ituri.
Wanamgambo hao waliteketeza nyumba zilizojaa raia, wakafyatua risasi na kuwakata vichwa wakazi katika vijiji hivyo huku wakiacha wengine na majeraha mbalimbali kwa mujibu wa chifu kijiji kimoja, wakili na mwanachama wa shirika la kutetea raia mnamo Jumanne.
Awali Jumapili usiku wanamgambo hao waliokuwa wamejihami kwa silaha kali walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani kabla kukabiliwa na Kikosi cha Walinda Usalama wa Umoja wa Mataifa Dr Congo (MONUSCO).
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/TF-DRC-1.jpg)
Mkuu wa vijiji hivyo vya Djaiba vinavyopatikana eneo la Djugu, Jean Vianney, alieleza kuwa wanamgambo hao wa CODECO walianza shambulio hilo mwendo wa saa mbili usiku Jumatatu na kuuawa takriban watu 52.
Kuna watu wamejeruhiwa, wengi wameteketezwa katika nyumba zao
Mbunge kutoka eneo la Djugu, Floribert Byaruhanga, alisema idadi aliyokukwa nayo ya watu waliofariki ni 51 wakati huo, wakiwemo watoto 18.
Nayo orodha ya mashirika ya kiraia Ituri ilionyesha kuwa watu 51 waliuawa usiku kucha kuanzia Jumatatu hadi Jumanne.
Aidha, mkazi wa Djaiba aliyenusurika mauaji hayo, Daniel Kisembo, aliambia Reuters kuwa alihesabu miili 51 mingi ilikuwa imeteketea.
Chimbuko la CODECO
CODECO ni mojawapo ya maelfu ya wanamgambo wanaopigania ardhi na rasilimali katika eneo pana la mashariki mwa DR Congo.
Waasi hao wanadai kupigania haki za jamii ya wakulima ya Lendu dhidi ya jamii ya wafugaji wa kuhamahama ya Hema.
Wameshutumiwa kwa kusababisha mauaji ya mamia ya raia tangu 2014, ambayo UN inakisia yanaweza kuwasilishwa kama makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Idadi kubwa ya wakazi katika eneo la Djugu ni wa jamii ya Hema.
Msemaji wa jeshi katika mkoa wa Ituri, Jules Ngono, alisema wanajeshi walifika wakiwa wamechelewa kuokoa wahasiriwa.
“Kilichotokea dhidi ya vijiji vya Djaiba ni maafa mabaya mno yaliyosababisha vifo vya watu wetu, na tunalaani kabisa,” alieleza Ngono kupitia simu.
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2025/02/TF-DRC-2.jpg)
Kwa upande wake, msemaji wa MONUSCO Jean-Tobie Okala alisema katika taarifa kwamba wanajeshi hao walifanikiwa kuwalinda watu waliokuwa katika kambi za wakimbizi dhidi ya waasi hao wa CODECO.
“Lakini wamebanwa hususan wavamizi wanapofurika kwa wingi kama walivyofanya jana usiku. Hili ni jambo la kusikitisha mno raia kuuawa wakiwa kambini. Hata hivyo, walionusurika wako salama,” akasema Okala.
Waasi wa M23
Haya yanajiri huku duru za kisiasa na kidiplomasia zikisema kuwa Afrika Kusini imetuma wanajeshi zaidi pamoja na zana za kijeshi eneo la mashariki mwa Congo, mwezi mmoja tu baada ya wanajeshi wake 14 kuuawa katika mapigano na waasi wa kundi lingine la M23.
Aidha, mashambulizi ya Ituri yanazidisha wasiwasi kuwa huenda mapigano yakasambaa na kuwa mabaya zaidi mkoa wa North Kivu ambako takriban raia 3,000 wanakisiwa kuuawa tangu Januari wakati waasi wa M23 waanzishe mapigano dhidi ya wanajeshi wa serikali ya DR Congo.
M23 imeteka mji wa Goma katika mkoa huo na kutangaza utawala wake.
Leave a Reply