
RAIS William Ruto amebadilisha nia na kuacha kuunganisha chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) na Amani National Congress (ANC) kwa kuhofia uasi, hasa kutoka kwa viongozi waliochaguliwa kutoka Mlima Kenya, Taifa Leo inaweza kufichua.
Badala yake, chama tawala cha Rais Ruto, UDA, kimemshawishi Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, kukivunja chama chake.Mabadiliko hayo yamo katika maazimio yaliyopitishwa na ANC katika Mkutano wake wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) uliofanyika Ijumaa, Februari 7 katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi.
Katibu Mkuu wa ANC anayeondoka Bw Omboko Milemba, aliambia Taifa Leo kwamba uamuzi huo ulihitajika ili kulinda UDA kuathirika kisiasa.’Tulikuwa na NDC yetu Ijumaa na tukakubali kuvunja ANC na kujiunga na UDA.
Kwa hivyo, sote tutakuwa katika UDA na huo ndio msimamo,’ alisema Bw Milemba, ambaye ameteuliwa kuwa naibu katibu mkuu wa chama tawala.
Aliongeza: ‘Kama tungeendelea na mpango huo ( kuungana) ungesababisha matatizo katika UDA.’Ufichuzi huo huo ulitolewa na mwenyekiti wa kitaifa wa ANC anayeondoka Bw Kevin Lunani, ambaye alisema uamuzi huo ulichochewa na nia ya kutaka kuunda upya UDA kabla ya uchaguzi wa 2027.’Tumekubali kuvunja ANC na kujiunga na UDA.
Kwa nini tuunde chama kipya wakati tuna chama tawala? Wanachama wetu sasa watakuwa wanachama wa UDA,’ alisema Bw Lunani, ambaye ameteuliwa kuwa naibu kiongozi wa UDA.
Kifungu kinachosimamia miungano ya vyama vya siasa kinatoa nafasi kwa wanachama ambao hawafurahishwi na makubaliano hayo kuhama.
Kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kinachoweka masharti ya miungano, kinasema viongozi waliochaguliwa, wanaopinga muungano, wana uhuru wa kuhamia vyama vingine vya siasa au kuwa huru.
“Pale chama kinapoungana chini ya kifungu hiki, mwanachama wa chama cha siasa ambacho kimeungana na chama kingine cha siasa atachukuliwa kuwa mwanachama wa chama kipya cha siasa,” kinasema kifungu cha 7 cha Sheria hiyo.
“Mwanachama ambaye ni Rais, Naibu Rais, Gavana au Naibu Gavana, Mbunge au Mwakilishi Wadi katika Bunge la Kaunti, na ambaye hataki kuwa mwanachama wa chama kipya cha siasa kilichosajiliwa baada ya muungano, ataendelea kuhudumu katika afisi aliyochaguliwa kwa muda uliosalia wa muhula, na anaweza kujiunga na chama kingine cha kisiasa au kuchagua kuwa mwanachama huru ndani ya siku thelathini baada ya kusajiliwa kwa chama kipya.
Kifungu hiki kingetoa fursa nzuri kwa washirika wa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua kuhama.
Leave a Reply