Kioja kortini mwanamke akimkodolea macho hakimu na kudinda kujibu mashtaka – Taifa Leo


MFANYAKAZI wa zamani wa shirika la serikali la kuzalisha nishati ya mvuke (GDC) aliibua kimya chenye mshindo mkuu mahakamani na kushangaza waliokuwamo.

Mwanamke huyo, aliyeshtakiwa kwa kutoa vitisho vya kumuua msimamizi wao, alishangaza Mahakama ya Milimani aliponyamaza kabisa na kukataa kujibu mashtaka sita aliyosomewa.

Hellen Nyambura Njoki alitoa kioja hicho  Alhamisi Novemba 28, 2024  alipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Gilbert Shikwe.

Jina lake lilipoitwa, Bi Njoki alinyanyuka na kuelekea kizimbani na kumtazama hakimu tu bila kuzungumza.

Bi Njoki aliposomewa mashtaka sita na kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech alikataa kuzugumza.

“Mheshimiwa,  mshtakiwa hataki kuzungumza. Sijui kama ameelewa mashtaka ama ameamua kunyamaza tu,” Bi Koech alimweleza hakimu.

Bw Shikwe aliamuru mshtakiwa asomewe mashtaka yote kisha aulizwe ajibu.

“Ni ukweli ama sio ukweli ulitisha kumuua Miriam Athmani Yunusi Aprili 13,2024 mahali pasipojulikana?” Bi Koech alimuuliza mshtakiwa.

Badala ya kujibu mshtakiwa alitazama kote mahakamani kisha akamkazia macho hakimu.

Mbali na shtaka hilo la kutisha kumuua Bi Yunus, pia Bi Njoki alishtakiwa kwa kumdhulumu mlalamishi kutumia njia ya mitandao.

Baada ya kumkodolea macho hakimu na kunyamaza alipoulizwa ajibu mashtaka ‘pengine kwa kuona haya kwa sababu yalikuwa ya aibu mno ama kwa kutoelewa mashtaka’ mahakama ilimweleza kwamba “itaandika amekanusha mashtaka.”

Bi Koech alimweleza hakimu hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bw Shikwe aliamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu.

Mahakama iliamuru kesi itajwe baada ya wiki mbili ili kutengewa siku ya kusikizwa.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*