
JOPO la kuteua mwenyekiti na makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) leo Jumatatu inaanza kuchambua jumla ya maombi 1, 848 kutoka kwa watu wanaotaka kujaza nafasi hizo.
Katika taarifa, mwenyekiti wa jopo hilo Nelson Makanda alisema kuwa baada ya shughuli hiyo kukamilika mwishoni mwa juma hilo, watachapisha majina ya wale walioorodheshwa kwa mahojiano.
“Kufikia mwisho wa muda wa kupokea maombi, Jumamosi Februari 15, 2024, tulikuwa tumepokea jumla ya maombi 1,848 kutoka kwa Wakenya wanaotaka kujaza nafasi saba za mwenyekiti na makamishna wa IEBC,” akasema.
“Kwa hivyo, kuanzia Jumatano, Februari 17, 2025 tutachambua maombi hayo kubaini ufaafu wa wanaotaka kujaza nafasi hizo kisha kuchapisha majina ya waliorodheshwa kwa usaili,” Dkt Makanda akaongeza.
Mwenyekiti huyo hata hivyo, hakubaini idadi ya watu waliotuma maombi ya kujaza nafasi ya mwenyekiti na idadi ya wale wanaotaka kujaza nafasi sita za makamishna wa IEBC, akieleza kuwa hilo litabainika baada ya zoezi la uchambuzi wa maombi kukamilika.
Dkt Makanda, kwa mara nyingine, aliwahakikishia Wakenya kuwa jopo hilo litazingatia haki, uwazi na uhitimu katika utekelezaji wa kibarua hicho.
Wiki jana, jopo hilo lilitangaza kuwa kufikia Aprili 25, 2025 litawasilisha kwa Rais William Ruto majina ya watu bora kwa nafasi za mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
“Tukiwasilisha majina kufikia Aprili 25, mwenyekiti mpya na makamishna sita wa IEBC watakuwa wemeingia afisini kufikia mwezi Mei mwaka huu,” naibu mwenyekiti wa jopo hilo Lindah Kiome akasema kwenye kikao na wanahabari Februari 7, baada ya mkutano wao mjini Naivasha.
Kulingana na Sheria ya IEBC ya 2024, jopo hilo litawasilisha, kwa rais, majina ya watu watatu bora kwa wadhifa wa mwenyekiti, kisha ateue mmoja wao.
Vile vile, Dkt Makanda na wenzake watawasilisha majina ya watu 14 kwa wadhifa wa makamishina ambapo Rais Ruto atateua sita kati yao.
Saba hao wataingia afisi kujaza nafasi iliyosalia wazi baada ya muda wa kuhudumu kwa aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishana watatu kutamatika mnamo Januari 17, 2023.
Nafasi nyingine nne zilisalia wazi Desemba 2022 baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna Wilfred Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya.
Leave a Reply