Mwanamume alivyojitia motoni akitaka mkewe aliyekamatwa aachiliwe huru – Taifa Leo


MAHAKAMA ya Kilifi imebaini jinsi mwanamume anayekabiliwa na kesi mbalimbali za ulaghai wa ardhi alivyojiingiza taabani baada ya mkewe kukamatwa.

Bw Nicholas Abongo aliwekwa kizuizini Februari 3, baada ya kuenda katika ofisi za Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) mjini Kilifi ambapo ilidaiwa alishambulia polisi akitaka mkewe, Bi Precious Mbindyo, ambaye alikamatwa siku moja awali, aachiliwe huru.

Bi Mbindyo alikamatwa wakati wapelelezi walipokuwa wameenda kumtafuta Bw Abongo lakini akatoroka.

Hii ilikuwa baada ya msajili wa ardhi wa Kilifi Billow Mohamed, kulalamika kwa DCI alipogundua jaribio la ulaghai wa ardhi ambalo lilidaiwa kufanywa na Bw Abongo mnamo Ijumaa, Januari 31.

Ijumaa iliyopita, Hakimu Mkuu wa Kilifi, Ivy Wasike, alikataa kumwachilia Bw Abongo kwa dhamana ya bondi wala pesa taslimu kufuatia maombi ya DCI kupitia kwa upande wa mashtaka.

Bi Wasike alisema upande wa mashtaka ulieleza kuwa, walikuwa na matatizo kumtafuta Bw Abongo kuhusiana na malalamishi yaliyotolewa dhidi yake.

Mahakama ilielezwa kuwa, ni hadi polisi walipomkamata mkewe ndipo alipokwenda kwa afisi za DCI na kuwashambulia na kuwajeruhi maafisa kwa nia ya kutaka mkewe aachiliwe.

Kwa mujibu wa Bi Wasike, ingawa mashtaka yake ni makosa makubwa, si sababu za kumnyima dhamana lakini mshukiwa alijidhihirisha kuwa mwepesi wa kutoroka na anayeweza kuwa tishio kwa mashahidi na walalamishi.

“Upande wa mashtaka ulisema kupitia kwa Afisa Mpelelezi kuwa, kumtafuta ni vigumu, na ni pale tu walipofanikiwa kumkamata mshtakiwa wa pili (Bi Mbindyo) ndipo alipokwenda kwa afisi ya DCI kumtaka aachiliwe na katika harakati hizo, kushambulia maafisa,” alisema.

Bi Wasike alieleza kuwa, mlalamishi katika kesi hii, ambaye ni mtu mwenye ulemavu, sasa anaogopa baada ya Bw Abongo kuenda katika afisi za DCI na kuwashambulia maafisa.

Hakimu alieleza kuwa, Bw Abongo hakuonyesha nia yoyote kwamba hataingilia mwathiriwa na mashahidi wanaomuogopa kwa sababu ya mwenendo wake.

Zaidi ya hayo, Bi Wasike alisema hajaonyesha wala kusema kwamba hatakiuka utulivu wa umma, amani au usalama.

“Mshtakiwa wa kwanza (Bw Abongo) yuko nje kwa dhamana katika masuala mengine lakini amefikishwa mahakamani kwa mashtaka katika suala hili, hali ambayo inaonyesha mienendo yake,” aliongeza.

Bw Abongo na mkewe Mbindyo walishtakiwa mapema wiki iliyopita kwa makosa 10 ya ulaghai na kujifanya wakili wa Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, tabia ya kihalifu ya Bw Abongo akiwa nje kwa dhamana katika kesi nyingine inazidi haki yake ya kuachiliwa kwa dhamana kwa sababu ya maslahi ya umma.

Hata hivyo, mke wake alipewa dhamana ya Sh250,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*