Jamani mume wangu ni mvivu ajabu,  nimechoka! – Taifa Leo


Vipi shangazi? Mume wangu ni mvivu sana kiwango cha kuwa ananiachia majukumu yote nyumbani, na hataki kujiendeleza kimaisha. Nimechoka!

Salama!Jaribu kujua kwa nini anashindwa kujihusisha na shughuli za kutafuta kazi. Ukishajua, mrekebishe kwa upole na ikiwezekana msaidie kupata kazi.

Baba wa kambo hataki watoto wangu

Shikamoo shangazi? Hivi majuzi niliolewa na huyu mwanamume baada ya mume wangu kufariki miaka minne iliyopita na kuniachia watoto wawili. Sasa nimeshika mimba yake na nimeanza kugundua ni kana kwamba hataki watoto wangu. Nifanyeje?

Marahaba! Ikiwa mwanamume huyo alikuoa akijua vyema kwamba una watoto, ana wajibu wa kuwapenda kama watoto wake. Zungumza naye kuhusu wasiwasi wako kwani ikiwa haya yataendelea, huenda ndoa yenu ikawa mashakani.

Mume amegundua nachovya asali yake na ametisha kunimaliza
Vipi shangazi? Kwa miezi kadhaa sasa nimekuwa katika uhusiano na  binti fulani mrembo, ambaye pia ni mke wa mtu. Hivi majuzi mumewe alidukua simu yake na kukutana na jumbe zetu za kimapenzi, na sasa ameanza kunitishia maisha. Nifanyeje?

Salama! Ikiwa unatishiwa maisha na unahisi kwamba usalama na maisha yako yamo hatarini,  itakubidi uandikishe taarifa katika kituo cha polisi. Lakini siku zote unapaswa kujua kwamba unapojihusisha na mume wa mtu unahatarisha maisha yako.

Nimegundua ana mke ila amenikwamilia tuendelee pembeni
Hujambo shangazi? Nimekuwa katika uhusiano na kaka huyu kwa miezi michache sasa. Mwanzoni sikujua kwamba ana mke lakini baadaye alikiri. Tatizo sasa ni kuwa hataki kuniacha. Anataka kuendelea na ndoa yake huku mimi kwa upande mwingine nikimpa burudani moto moto pembeni. Nikubali?

Sijambo! La hasha! Maisha ya kaka huyo yanaendelea huku yako yakiwa yamesimama katika uhusiano huu usioeleweka. Kando na hayo, unajiweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa na hata kushambuliwa na mkewe.

 

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*