Ruto aangalia Nyanza kuliko msaada wake 2027 – Taifa Leo


JUHUDI za Rais William Ruto kuweka thabiti azma yake ya kuchaguliwa tena 2027 zimeanza kuzaa matunda eneo la Nyanza.

Hii ni baada ya wakosoaji wake ambao ni wafuasi sugu wa Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kuanza kumpigia debe.

Miongoni mwa viongozi wa hivi karibuni zaidi kumuunga mkono ni Waziri wa Hazina ya Kitaifa John Mbadi ambaye aliwarai wapigakura wa Nyanza kumchagua Dkt Ruto 2027.

Akizungumza alipozuru Suba Kusini, Bw Mbadi alisifu serikali ya Kenya Kwanza na kuhakikishia wakazi kuwa iwapo watamuunga mkono Rais, hatua hiyo itachochea eneo lao kimaendeleo.

Huku Bw Raila Odinga akiwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Bw Mbadi, ambaye alikuwa mkosoaji mkali wa Rais Ruto, anasifu uongozi wake katika eneo ambalo liliunga mkono mpinzani wake (Raila Odinga) kwa kura nyingi.

“Nitashindwa kuamua ni nani nitaunga mkono iwapo Raila Odinga na Rais Ruto watawania urais 2027,” akasema Waziri Mbadi.

Waziri huyu ni kati ya maafisa wakuu wa serikali ambao wanapigia debe ajenda ya serikali.

Wakati uo huo, wanawasihi wakazi wa kanda ya ziwa kumchagua tena Rais katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Acheni eneo hili lipuuze mwaniaji mwingine wa urais endapo Raila Odinga hatakuwa akigombea,” akasema.

Bw Mbadi alizungumza baada ya kutawazwa na wazee kuwa msemaji wa Nyanza kuhusiana na masuala ya siasa za kitaifa.

Hafla hiyo ilifanyika katika Shule ya Msingi ya Kitawa mnamo Ijumaa ili kusaidia Shirika la Wasomi wa Kobunda.

Wazee wa eneo hilo walihudhuria na kumpongeza Bw Mbadi kwa kuwaongoza alipokuwa mbunge.

Wakongwe hawa wanaamini waziri huyu atakuwa muhimu kwa jamii hii kwa kutoa mwelekeo bora wa kisiasa.

Rais Ruto, ambaye aliahidi kufanikisha usawa wa kimaendeleo, alitaja kuwa eneo la Nyanza lilimpinga sana katika uchaguzi wa 2022, lakini akaapa kuhakikisha eneo hilo linanufaika kimaendeleo kutoka kwa serikali yake.

Kulingana na Waziri Mbadi, uamuzi wake wa kumuunga mkono Dkt Ruto ulitokana na ukweli kwamba Rais pia alimuunga mkono Bw Odinga mnamo 2007 alipokuwa Waziri Mkuu.

“Eneo zima la Bonde la Ufa lilituunga mkono 2007. Jamii yetu inafaa imuunge mkono Rais Ruto katika uchaguzi ujao,” alisema.

Alipokuwa akihutubu, Bw Mbadi alisema Rais Ruto anapenda Nyanza na kwamba serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itabadilisha maisha ya wakazi.

Baadhi ya miradi aliyoitaja ni pamoja na kuweka lami barabara ya Mbita-Sindo-Magunga-Sori yenye urefu wa kilomita 73, barabara ya Ziwa Victoria pamoja na miradi mingine ya maendeleo.

“Tunatarajia kupata manufaa zaidi kutoka kwa serikali. Kwa hivyo tuendelee kuunga mkono serikali jumuishi,” Bw Mbadi alisema.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*