
MAHAKAMA ya Bomet Jumatatu ilimhukumu mwanaume kutoka kijiji cha Magutek, Kaunti ya Bomet, kifungo cha miaka 150 jela kwa kuua watoto wake watatu.
Jaji Julius Kipkosgei alimhukumu Benard Kirui Kipkemoi adhabu hiyo kali baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wanawe hao mnamo Machi 20, 2019.
Kipkemoi alikuwa amezozana na mkewe Sharon Cherono usiku wa Machi 18, 2019. Tukio hilo lilisababisha atoroke na wanawe Amos Kipngetich, 11, Vincent Kiprotich, 8, na Emmanuel Kiprono, 5.
Mumewe Cherono alimfuata siku iliyofuata ya Machi 19 na akiwa amelewa alitaka apewe wanawe arejee nao kwake ili waende shuleni.
Kwa kuwa usiku ulikuwa umefika, aliambiwa wangeruhusiwa waende kwake siku iliyofuata.
Bi Cherono aliwatuma watoto hao na hiyo ikawa mara ya mwisho kuwaona wakiwa hai. Usiku huo wa Machi 20, baba yao aliwageuka na kuwatia kitanzi.
Tukio hilo la kuatua moyo liligunduliwa asubuhi iliyofuata na nyanya ya watoto ambaye alipata miili yao ikiwa imefunikwa kwa blanketi.
Alipiga nduru, na majirani waliofika walipata kamba mbili zikiwa zilitumika kuwatia kitanzi.
Miili ya watoto hao ilipelekwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti huku msako wa kumtafuta baba yao ukianza. Uchunguzi wa upasuaji maiti uliofanywa na Dkt Nickson Mutai ulithibitisha kuwa watoto hao waliaga dunia kwa kukosa hewa kutokana na kunyongwa.
Kipkemoi baadaye alikamatwa na kufufunguliwa mashtaka matatu ya mauaji mnamo Aprili 25, 2019 lakini akakanusha mashtaka hayo.
Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, mashahidi wanne walikuwa kortini kuunga mashtaka dhidi yake huku naye akijitetea mwenyewe.
Kipkemoi kwenye utetezi wake alisema aliwaacha watoto hao pekee yao saa 12 jioni siku hiyo.
Aliongeza kuwa alirudi asubuhi iliyofuata na kupata wameaga dunia. Wakati wa kuhojiwa na mawakili, alikiri kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na watoto hao.
Pia alikosa kufafanua kwa nini alikuwa ametoroka kabla ya kukamatwa kwake. Licha ya mashtaka dhidi yake, alisisitiza hakuwa na sababu yoyote ya kuwaumiza watoto wake huku akishikilia kuwa hakutenda uhalifu huo.
Mnamo Novemba 23, 2023, korti ilitoa uamuzi kuwa alikuwa na kesi ya kujibu. Jaji Lagat Korir alipuuza utetezi wake, akisema hakuwasilisha shahidi ambaye angethibitisha hakuhusika na mauaji hayo.
“Sijapata ushahidi wowote au uwezekano kuwa mtu mwingine huenda aliwaua watoto hao. Kutokana na ushahidi uliowasilishwa, ni dhahiri kuwa mshtakiwa alitekeleza mauaji hayo,” akasema Jaji Korir.
“Ushahidi unaonyesha kuwa mshtakiwa aliwaua watoto wake na kusababisha vifo vyao. Aliwaua usiku mahali waliyoita nyumbani na mauti hayo yalisikitisha sana,” ikaongeza sehemu ya uamuzi wa Jaji Korir.
Jaji huyo pia alilalamikia kuongezeka kwa visa vya dhuluma za nyumbani na kutoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, yale ya serikali, makundi ya kidini na viongozi, waungane kupambana na dhuluma hizo ili kuzuia maisha kupotea.
“Kwenye utathmini wangu wa mwisho, upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka ya mauaji dhidi ya mshtakiwa. Mauaji ya watoto hao watatu yalitekelezwa na mshukiwa,” akasema kwenye uamuzi wake.
Alisema tukio hilo halikuzingatia ubinadamu na lilisikitisha mno. Hukumu hiyo inalenga kuwa kama onyo kwa wenye nia ya kutenda uhalifu kama huo.
“Mahakama hii haiwezi kupuuza tukio la unyama kama huu. Adhabu lazima iwe kali kuwiana na uhalifu uliotekelezwa,” akaamua.
Leave a Reply