
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amemrai Kinara wa ODM Raila Odinga agure kambi ya Rais William Ruto na aungane nao kupinga utawala wake kisha kumng’oa madarakani mnamo 2027.
Bw Musyoka amemtaka Bw Odinga arejelee siasa zake za upinzani na kutetea raia badala ya kujiunga na utawala wa Rais Ruto ambao umefanya maisha yawe magumu zaidi kwa raia.
Mnamo Jumatano, Bw Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa waliandaa mkutano Nairobi ambapo suala la ushirikiano kati yao lilijadiliwa kwa mapana na marefu.
“ODM ndio ina ufunguo na udhabiti kwa utawala wa Rais Ruto. Raila lazima aamue na ajitokeze wazi kupambana na dhuluma dhidi ya Wakenya badala ya kuwaachia washirika wake kama Junet Mohamed kuzungumzia masuala ya serikali,” akasema Bw Musyoka.
“Anastahili kurejelea siasa za maasi jinsi alivyokuwa akifanya zamani akipigania demokrasia. Inashangaza kuwa sasa yuko radhi kupoteza yote aliyoyapigana kwa kujiunga na serikali ya udikteta ya Kenya Kwanza. Akijiunga na Rais Ruto, atapoteza,” akaongeza Bw Musyoka.
Kiongozi huyo alikuwa akiongea kwenye mahojiano na runinga ya KTN ambapo alisema baada ya kushindwa kwenye kura ya uenyekiti wa Tume ya Afrika (AUC) Raila ana hiari ya kujiunga na serikali au kurejea upinzani.
“Akirejea upinzani atakuwa amejiokoa na kurejesha hadhi yake, akikosa kufanya hivyo, basi atapoteza,” akasema.
Bw Musyoka alikuwa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga katika chaguzi za 2013 na 2017 lakini walipoteza kwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Ruto ambaye wakati huo alikuwa mgombeaji mwenza wa Bw Kenyatta.
Katika uchagauzi wa 2022, Bw Musyoka alikosa kuwa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga lakini bado akamuunga mkono japo wawili hao walipoteza kwa Rais Ruto.
Bw Musyoka alimtaka waziri huyo mkuu wa zamani kuweka maslahi yake ya kibinafsi kando na aungane nao kwenye juhudi za kuwakomboa Wakenya kutoka kwa Rais Ruto.
Alisema kuwa wakati ambapo Raila alikuwa kwenye kampeni AUC, waliendesha upinzani vyema na kuzima serikali kuendelea na dili Adani akisisitiza kuwa hoja kuu kwa sasa ni kuhakikisha ushuru ambao wafanyakazi wanatozwa unapunguzwa.
Tangu kupoteza AUC kumekuwa na wito wa Bw Odinga kujumuishwa serikalini ili apate wadhifa wa waziri mkuu lakini Bw Musyoka anasema huko kutakuwa ni kuwasaliti Wakenya.
“Kwa maneno yetu na yake pamoja na wafuasi wetu, tunaamini Raila alishinda uchaguzi wa 2022. Kwa hivyo, itakuwa aje awe waziri mkuu katika serikali ya mtu ambaye alimpiku kwenye uchaguzi huo?” akahoji.
Aidha alimkumbusha kuwa Kamati ya Haki juzi iliamua kuwa hakuna uwezekano wowote wa kubuniwa kama wadhifa huo wa waziri mkuu.
“Wasifu wa Bw Odinga haumruhusu kuwa waziri mkuu katika utawala wa Rais Ruto. Akijiunga naye, basi atakuwa ameasi kabisa msingi wa kubuniwa kwa Kamati ya Maridhiano (NADCO),
“Ripoti hiyo ilikuwa na nia ya kuwapatanisha na Ruto na akijiunga naye, atakuwa amepoteza,” akasema.
Bw Musyoka pia alimwendea Rais Ruto kwa maneno makali akimlaumu kwa kutumia vyombo vya usalama baada ya uchaguzi wa 2022 kukabili upinzani.
Aidha alisema sifa hasi ambazo Rais anazo machoni pa Umoja wa Kimataifa ndizo zilisababisha Bw Odinga kushindwa katika kura za AUC.
“Tuna serikali ambayo haina ujuzi wowote kuhusu masuala ya kigeni na kidiplomasia. Hii serikali haiheshimu sheria ya kutoingilia mataifa mengine, Ruto amevuruga EAC na heshima ambayo tulikuwa nayo kwenye nchi za IGAD,” akasema.
Kando na Mabw Gachagua na Wamalwa, Bw Musyoka pia analenga kuwa na muungano na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Seneta wa Busia Okiya Omtatah, Seneta wa Kisii Richard Onyonka na waziri wa zamani wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiangí.
Leave a Reply