UCHUNGUZI kuhusu mauaji ya kinyama ya mgonjwa aliyelazwa katika hospitali kuu ya Kenyatta, KNH, huenda ukachukua mkondo usiotarajiwa huku mgonjwa mwenza aliyekuwa wadi moja na mhasiriwa akiangaziwa.
Mwili wa Bw Gilbert Kinyua ulipatikana akiwa amekatwa shingo kitandani mwake katika Wadi 7B kitengo cha wanaume, katika tukio hilo lililoibua taharuki kuhusu usalama wa wagonjwa nchini.
Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya inayochunguza mauaji hayo ilifahamishwa mgonjwa huyo ambaye hajatambulishwa, alikuwa ameruhusiwa kuondoka hospitalini mhasiriwa alipouawa kikatili Februari 7.
Licha ya kutibiwa na kupatiwa kibali cha kuondoka, mgonjwa huyo aliyeugua kisukari na kifafa, aliendelea kukaa hospitalini baada ya waliokuwa wakimtunza kumkataa wakitaja ‘mienendo yake isiyofaa”, ilisikia Kamati.
“Ni mgonjwa wetu wa muda mrefu na hana makao. Alikuwa ametibiwa kuhusiana na kisukari na kifafa lakini hali yake haingemruhusu aondoke,” alisema Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu KNH, Dkt William Sigilai.
Dkt Sigilai alifichua kwamba,” Tulimtafutia makao kupitia mmoja wa washiriki wetu kwa sababu tuna wagonjwa kadhaa wasio na makazi hapa KNH.”
Alama za vidole za mgonjwa huyo zimepelekwa kwa Shirika la Kitaifa la Usajili na suala hilo kwa sasa lipo mikononi mwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kulingana na Dkt Sigilai.
Kundi la wabunge linamtaka mgonjwa huyo aliyekuwa U na mhasiriwa aliyeuawa aangaziwe katika uchunguzi unaondelea.
“Ninavutiwa na mgonjwa huyu. Hali yake iko vipi kiakili? Aliugua kisukari na kifafa,” alisema Mbunge wa Seme, James Nyikal.
“Mimi na wewe tunajua kifafa sio tu kutetemeka mwili lakini wakati mwingine ugonjwa huo hujitokeza kama tabia usiyoweza kujizuia, hali ambapo mtu hufanya kitendo bila kukumbuka baadaye.”
Haya yalijiri huku ziara iliyofanywa na Kamati ya Afya inayoongozwa na Mbunge wa Endebbes, Robert Pukose, kufichua hali ya kushtusha kuhusu ulegevu kwenye mifumo ya usalama wa ndani katika hospitali kubwa zaidi ya rufaa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati alisema japo KNH imeimarisha usalama unaozuia tishio kutoka nje ikiwemo kituo cha polisi kituoni humo, usalama wa ndani kwa wagonjwa na wahudumu wa afya haujazingatiwa.
Dr Pukose alitaja ukosefu wa mikakati ya kuwakagua watu wanaoingia na kutoka viingilioni licha ya hospitali hiyo kupokea maelfu ya watu wakati wa saa za kuwatembelea wagonjwa hali inayohatarisha wagonjwa na wahudumu.
“Tulihisi ni muhimu kama sehemu ya wajibu wa Kamati kufanya ziara ya udadisi kuhusu usalama wa hospitali kuhusiana na tishio zinazotokana na ndani na nje, wagonjwa wetu wako salama kwa kiwango gani wanapokuwa hapa,” alieleza Dkt Pukose akihutubia vyombo vya habari baada ya ziara ya Udadisi Ijumaa.
“Ripoti ambayo tumepokea kutoka hospitali inaashiria kuna eneo linalohitaji kurekebishwa hasa upande wa ndani ili usalama uimarishwe,” alisema.
“Mikakati ya kulinda usalama wa waliomo ndani kama vile kuweka vituo vya ukaguzi viingilioni ili kuwakagua watu na mifuko ya wanaoingia hospitali.”
“Hiyo ni sehemu tunayoweza kusaidia KNH kuhakikisha wana ukaguzi huo kwa sababu kwa wakati wowote watu wapatao 30,000 hutembelea hospitali hiyo. Haiwezekani kuwarekodi wote lakini inawezekana kuwaagiza wapitie kifaa hicho cha ukaguzi ili kusiwe na atakayeleta silaha.”
Kuhusiana na mgonjwa mwenza aliyelazwa pamoja na mhasiriwa, Bw Pukose alisema,”Nitarihusu DCI kufanya kazi yao. Tutahifadhi maoni yetu ili turuhusu mashirika yetu kufanya kazi yao. Hatutaki kuvuruga uchunguzi.”
Leave a Reply