Ombi Wakenya wapendekeze njia ya kuboresha ufadhili wa elimu vyuoni – Taifa Leo


WIZARA ya Elimu inaomba Wakenya watoe maoni yao kuhusu mfumo mpya wa ufadhili wa elimu vyuoni.

Wakenya wanatakiwa kupendekeza njia ya kuboresha mfumo huo ambao umeibua utata tangu uanzishwe.

Katibu wa Idara ya Elimu ya Vyuo na Utafiti Dkt Beatrice Inyangala amesema kamati inayokusanya maoni iko tayari kuwasikiliza wananchi.

“Serikali imejitolea kuwapa wanafunzi elimu nafuu na inayofaa wakati wote. Ni kwa sababu hii kamati iliundwa kuangazia masuala yaliyoibuliwa kuhusiana na mfumo wa ufadhili wa elimu vyuoni,” akasema.

Kulingana na Wizara ya Elimu, mfumo mpya unahakikisha kuwa kila mwanafunzi anasaidiwa kwa kutumia kigezo cha uhitaji kutegemea na mshahara wa familia.

Kuliibuka cheche kali na maandamano kutoka kwa Wakenya baada ya mfumo wa ufadhili kuwaweka wanafunzi katika kundi lisilofaa huku wengine wakiteta walipokea msaada mdogo zaidi kuliko waliotarajia.

Ilibidi serikali iunde kamati ya kukusanya maoni na kupendekeza marekebisho.

Jopo hilo linajumuisha viongozi wa wanafunzi, makamu chansela wa vyuo, wahadhiri na wataalamu wengine pamoja na wananchi wa kawaida.

“Hii ni serikali ambayo husikiliza na tumewasikia. Tutaendelea kuwasikiliza,” akasema Dkt Inyangala.

Katibu huyu amesema malalamishi ya wanafunzi yanaweza kutumwa kwa wakuu wa vyuo na viongozi wa wanafunzi.

“Tunategemea mawazo yenu ya ubunifu kuboresha mfumo wa ufadhili ili ukithi mahitaji ya kila mmoja,” alisema mnamo Ijumaa alipohudhuria hafla ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya mjini Homa Bay.

Alitetea mfumo huo akisema ulianzishwa kusaidia wanafunzi na wazazi kutegemea hali za kiuchumi za familia.

“Lengo lake lilikuwa kusambaza fedha za kutosha kwa vyuo vikuu kuimarisha viwango vya elimu,” akaongeza akisema mfumo huo ulitekelezwa kikamilifu katika mwaka wa kwanza kabla ya malalamishi kuibuka.

Mfumo huu ulianzishwa mnamo Mei 3, 2023 na umekumbwa na pingamizi baada ya wanafunzi wengi kutengewa migao midogo.

Utaratibu wa ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo unahusisha mseto wa ufadhili kutoka kwa serikali, mikopo na karo.

Rais William Ruto alibuni kamati ya wanachama 129 mnamo Septemba 16, 2024 kupiga msasa mfumo huo kwa kipindi cha angalau wiki nane.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*