Kamwe hatufai kucheza karata na sekta ya afya jinsi hali ilivyo – Taifa Leo


IJUMAA, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura aliwataka madaktari kurejea katika meza ya mazungumzo akielezea kujitolea kwa serikali kushughulikia malalamishi yao.

Ilishangaza Bw Mwaura kutoa wito huo siku chache baada ya Chama cha Kutetea Maslahi ya Madaktari Nchini (KMPDU) kuahidi kuitisha mgomo mwezi huu wa Desemba, baada ya serikali kufeli kutimiza ahadi yake ilivyo kwenye mkataba wa kurejea kazini uliotiwa saini Mei 8 mwaka huu.

Kulingana na mkataba huo uliositisha mgomo wa madaktari wa siku 56, serikali ilifaa kuongeza mishahara ya madaktari wanagenzi na marupurupu ya madaktari wengine kando na kuimarisha mazingira yao ya kazi.

Lakini miezi sita baadaye serikali bado haijatimiza ahadi hiyo, hali inayochangia madaktari wanagenzi kuendelea kuteseka wakilazimika kufanya kazi kwa saa nyingi huku mishahara yao duni ikicheleweshwa.

Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt Davji Bhimji Atellah (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Dkt Dennis Miskellah katika kikao na wanahabari kuwasilisha matakwa mbalimbali kwa serikali, mnamo Januari 31, 2023. Atellah ameahidi kuitisha mgomo tena kwani matakwa yao bado hayajatimizwa. PICHA | LUCY WANJIRU

Masaibu hayo ya kikazi na kifedha yamesukuma baadhi kujitoa uhai waliposhindwa kustahimili.

Kwa mfano, Desree Moraa aliyekuwa akihudumu katika hospitali ya Gatundu Level 5 na Francis Njuki aliyekuwa akihudumu katika hospitali ya Thika Level 5, walithibitishwa kujiua kutokana na masaibu waliyokuwa wakipitia kazini.

Hii ndio maana wiki jana Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah aliagiza madaktari wanagenzi kususia kazi huku akiahidi kuitisha mgomo mwingine wa madaktari wote  Desemba hii.

Kile serikali inapaswa kufanya sio kuwaita madaktari kwenye meza ya mazungumzo bali kutekeleza makubaliano ya Mei 8, 2024. Si haki kwa madaktari wanagenzi kulipwa mshahara wa Sh70,000 huku wakifanya kazi katika mazingira magumu na kwa saa nyingi kupita kiasi. Isitoshe, mshahara wenyewe hucheleweshwa kwa hadi miezi minne!

Kulingana na Dkt Atellah wengi wa madaktari hao hulazimika kufanya kazi kwa zamu zinazodumu saa 36 na katika hospitali zisizokuwa na vifaa tosha vya matibabu.

Wakazi wakisaka huduma za afya katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Coast General mjini Mombasa, wakati wa mgomo wa madaktari Aprili 2024. Utoaji huduma ulipungua kutokana na mgomo. PICHA | KEVIN ODIT

Agizo la KMPDU kwa madaktari hao kwamba wasusie kazi linaathiri pakubwa shughuli katika hospitali za umma za kuanzia kiwango cha Level 4 hadi juu Level 6.

Hii ni kwa sababu ni kwamba matabibu hao ndio hutegemewa zaidi kutoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali hizo.

Kimsingi, kutokuwepo kwa madaktari wanagenzi bila shaka kutawatumbukiza wagonjwa katika lindi la mahangaiko makubwa wakati huu ambapo utekelezaji wa Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF) pia umezongwa na changamoto si haba.

Wakazi wakisaka huduma za katika eneo lingine la hospitali ya Coast General wakati wa mgomo wa madaktari mwezi Aprili 2024. PICHA | KEVIN ODIT

Serikali ya Rais William Ruto isiposhughulikia matakwa ya madaktari, kama yalivyo kwenye makubaliano kati yake na KMPDU, basi utekelezaji wa SHIF utafeli kabisa.

Inavunja moyo kwamba serikali imekuwa ikitumia muda na pesa nyingi kufanikisha ajenda za kisiasa huku ikisusia kutekeleza jukumu muhimu la kuimarisha maslahi na mazingira ya kikazi ya wahudumu wa afya.

Malengo ya Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) hayatatimizwa ikiwa serikali haitatimiza jukumu hilo kwani madaktari hao ndio watendaji halisi wa mpango huo ulio mojawapo ya ajenda kuu za maendeleo katika utawala wa Rais Ruto.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*