
HOSPITALI ya Kitaifa ya Mafunzo na Rufaa ya Mathari (MNTRH) imejaa wagonjwa waliopona matatizo ya kiakili ila wamekwama hapo, baadhi kwa zaidi ya miaka 40, Kamati ya Afya ilielezwa.
Ukosefu wa taratibu za kisheria, mchakato uliojaa vizingiti chungu nzima, na changamoto katika taratibu za usimamizi na Idara ya Mahakama zimesababisha mamia ya wagonjwa waliopona kukwama katika hospitali hiyo kubwa zaidi ya kutibu maradhi ya akili kanda ya Afrika Mashariki.
Afisa Mkuu Mtendaji wa MNTRH Dkt Julius Ogato alifichua hayo katika kikao na Kamati ya Bunge kuhusu Afya inayoongozwa na Mbunge wa Endebbes, Robert Pukose, Jumatano.
Dkt Ogato alilalamikia kuwepo mchakato mrefu kupindukia ambao umewaacha Wakenya wengi wakiwa wamekwama katika hospitali ya matatizo ya akili na sintofahamu kuhusu siku zao za usoni miaka mingi baada ya kupata afueni.
Wagonjwa hao walipelekewa na kulazwa hospitalini humo mwanzoni kupitia amri ya mahakama baada ya vipimo kuashiria hawana urazini wa kujibu mashtaka ya uhalifu.
Kulingana na Dkt Ogato, ili wagonjwa kama hao waachiliwe huru ni sharti kutolewe kibali cha korti, lakini kinachukua muda mrefu sana sababu ya kujikokota kwa mchakato wa utoaji idhini wa mahakama.
“Hata tuna mgonjwa aliyeletwa hapa (Mathari) kwa miaka 40. Baadhi wamepona kiakili lakini hatuwezi kuwaachilia. Kuna pengo la kisheria. Walio na uwezo wa kiakili wanakaa hospitalini mwetu maisha yao yote,” alieleza Dkt Ogato.
Alisema: “Tuna wagonjwa kadhaa walio wazima kabisa lakini hatuwezi kuwaruhusu kuondoka pasipo kibali za sheria kwa sababu waliletwa hapa kupitia amri ya korti.
“Mchakato huo huchukua muda mrefu sana kwa sababu ya changamoto za taratibu kwenye mfumo wa usimamizi na mahakama.”
Kwa sasa wahalifu ambao ni watoto au wasio na akili timamu ya kujibu mashtaka hupewa vifungo vya muda usiojulikana gerezani.Kisheria, wanatumikia kifungo cha jela kwa muda anaoruhusu Rais; hatma yao ipo mikononi mwa Kamati ya Ushauri kuhusu Huruma (POMAC).
Kamati hiyo imetwikwa mamlaka na Kifungu 133 cha Katiba na Sheria kuhusu Nguvu za Huruma.Wajibu wake ni kutathmini kesi zinazohusu kuachiliwa kwa watu waliofungwa jela hadi kwa muda atakaoamua Rais. Washtakiwa wanaofaulu husamehewa kupitia notisi rasmi.
Baadhi ya majaji wa Mahakama Kuu katika hukumu za awali wamekosoa mtindo wa kuwafunga jela watu kwa hiari ya Rais wakihoji kuwa inaingilia uhuru wa idara ya mahakama na kwamba vifungo vya muda usiojulikana vinakiuka haki za wafungwa.
Alipofika mbele ya wabunge wakati wa kupiga msasa Taarifa ya Sera kuhusu Bajeti 2025/2026, Dkt Ogato alisema hali ya wafungwa kukaa jela kwa muda mrefu kuliko inavyofaa imewezeshwa na pengo lililopo huku Idara ya mahakama ikiwazuilia washukiwa au wafungwa walio na matatizo ya kiakili kupitia amri ya korti pasipo mifumo ya kuwaachilia huru.
Mkuu wa Hospitali ya Mathari alitaja ukosefu wa mfumo wa kisheria unaoharakisha mchakato wa kuachilia kuwa sababu wagonjwa kadhaa wangali wanataabika katika hospitali hiyo kwa miongo kadhaa hata baada ya kukamilisha matibabu yao.
“Tunahitajika kisheria kusubiri hadi korti inapotoa amri au uamuzi. Mfumo wa mahakama unajikokota na wakati mwingine kesi hazifuatiliwi baada ya kuletwa.”Kauli ya afisa huyo ilijiri huku maafisa wa hospitali, wabunge na watetezi wa afya ya kiakili kuelezea wasiwasi wao kuhusu wagonjwa kuzuiliwa kwa muda mrefu zaidi ya muda unaohitajika kwa matibabu yao.
Wanahoji kurefushwa kwa muda huo, kando na kuongezea mzigo kituo hicho cha afya ya kiakili ambacho tayari kinakabiliwa na uhaba wa raslimali, kunakiuka haki na uhuru wa wahusika.
Mtu anaweza kupelekwa Mathari kupitia agizo la mahakama. Kipengee 11 cha Sheria kinasema kila mtu hudhaniwa kuwa na akili timamu hadi ushahidi unathibitisha kinyume unapowasilishwa.
Leave a Reply