Mackenzie akemea wanaodai ameaga dunia – Taifa Leo


MSHUKIWA wa mauaji ya Shakahola, Bw Paul Mackenzie, amekashifu vikali uvumi ulioenea mitandaoni kwamba amefariki na kuutaja kama uongo na wenye nia mbaya.

Akizungumza kupitia wakili wake Lawrence Obonyo, mhubiri huyo alisisitiza yu hai na mwenye afya njema.

“Tumesikitishwa sana na uvumi huu, una nia mbaya. Hatujui sababu lakini tunahisi kuna mtu fulani ana nia nyingine. Mackenzie yu hai na ana afya njema,” alisema Bw Obonyo alipoandamana na mshukiwa huyo pamoja na wengine katika Mahakama ya Tononoka.

Bw Obonyo alidokeza kuwa washtakiwa wawili tayari wamefariki dunia wakati wa kesi hiyo akisema uvumi wa kifo unaathari kubwa kwa washtakiwa, familia zao, na waathiriwa.

‘Taarifa si nzuri kwa familia yangu’

“Taarifa kama hizi si nzuri kwa familia za walio gerezani. Tunaomba Mackenzie na washtakiwa wengine wasipatwe na lolote hadi kesi hii itakapokamilika,” alihoji.

Wakili huyo aliwataka Wakenya kumuacha Mackenzie apitie mchakato wa sheria bila kumshambulia kiholela, akisisitiza mteja wake hana hatia hadi itakapothibitishwa kortini.

Mwisho wa juma lililopita uvumi ulienea katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Mackenzie, hali iliyomfanya Wakili Obonyo kujitokeza kukayana na kusisitiza mshtakiwa yu hai.

Tukio hilo lilijiri huku Mahakama Kuu ikisimamisha kwa muda kesi ya Mackenzie na wenzake 38 katika Mahakama ya Watoto ya Tononoka, kufuatia ombi la Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kupinga uamuzi wa mahakama kukataa kuahirisha kesi hadi Februari 2025.

Usikilizaji wa kesi

Jaji Wendy Micheni alitoa amri mnamo Alhamisi wiki jana kusimamisha usikilizaji wa kesi hiyo katika Mahakama ya Watoto.

“Mahakama hii inataka rekodi za kesi ili kudhibitisha usahihi, uhalali na utiifu wa kanuni katika maamuzi ya korti yaliyotolewa Novemba 25 na 27, pamoja na mwenendo wa kesi,” alieleza Jaji Micheni wa Mahakama Kuu.

Katika maamuzi hayo mawili, Hakimu Mkuu Nelly Chepchirchir wa Mahakama ya Watoto ya Tononoka alikataa kuahirisha kesi hiyo hadi Februari mwaka ujao kama ilivyoomba ODPP.

Hakimu Chepchirchir akieleza kusita kwake kukubali ombi hilo, alisema kwamba kuchelewesha kesi kungeathiri waathiriwa na washtakiwa.

“Viongozi wa mashtaka wanaweza kuendesha kesi hii kutoka ofisini mwao kwa njia ya mtandao, sio lazima wasafiri hadi Mombasa,” alihoji Hakimu Chepchirchir na kuamuru kesi iendelee baada ya kuiahirisha kwa siku mbili tu.

Hata hivyo, ODPP iliwasilisha shahidi mmoja tu kabla ya kuishtaki Mahakama ya Bi Chepchirchir katika Mahakama Kuu akitaka kuzuia kesi hiyo kuendelea.

Mackenzie na wenzake 38

Kesi iliratibiwa kuendelea kesho na Alhamisi ambapo Mackenzie na wenzake 38 wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo mateso na ukatili dhidi ya watoto, pamoja na ukiukaji wa Sheria ya Elimu ya Msingi.

Katika ombi lake mbele ya Jaji, Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma wa Mombasa, Bw Peter Kiprop, ameomba jaji aamue kuwa maamuzi ya mahakama ya watoto yalikuwa si sahihi, si halali, na hayakuzingatia sheria.

Bw Kiprop alidai kuwa, upande wa mashtaka ulitoa sababu za kutosha za kuomba kesi hiyo ihairishwe mnamo Novemba 25 na 27, na hivyo ombi lao lilikuwa na msingi wa kisheria.

“Tuliweka maombi hayo kwa msingi kuwa ofisi ya ODPP inapitia changamoto ya kifedha hivyo imekuwa vigumu maafisa wake kufika Mombasa kuendelea na kesi kama kawaida. Jambo hili linashugulikiwa kwa hivyo tunaomba muda ndio tuweke kuwa tayari kuendelea,” alisema.

Ugumu na uzito wa kesi

Kulingana na ODPP, ugumu na uzito wa kesi hiyo unahitaji timu maalumu ya waendesha mashtaka saba, lakini changamoto za kifedha na uhamisho zimevuruga mpango huo.

“Ni kwa manufaa ya umma kwamba upande wa mashtaka upewe fursa ya kuendesha kesi hii ya jinai angalau kwa kuwa na mmoja wa waendesha mashtaka wakuu akihudhuria mahakamani moja kwa mojai,” alisema Bw Kiprop.

Katika kesi hii, Mackenzie na wenzake 38 wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali, yakiwemo mateso na ukatili dhidi ya watoto, pamoja na ukiukaji wa Sheria ya Elimu ya Msingi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*