
IDARA za usalama katika Kaunti ya Homa Bay zinachunguza jinsi mauti ya mvuvi mmoja yalivyotokea akidaiwa alizama baada ya kutoka kwenye boti akivua samaki katika ufuo wa Angalo, Jumamosi.
Marehemu John Okombo, 43, alifariki alipokuwa akivua samaki na nduguke saa tatu asubuhi.
Mwili wake ulipatikana saa chache baadaye, baada ya msako uliofanywa na wavuvi wengine kutoka ufukwe jirani.
Nduguye marehemu, Bw Peterlis Ooko, alisema kuwa Bw Okombo alikuwa na tatizo la kiafya ambalo huenda lilichangia kifo chake.
Aliongeza kuwa kakaye alishindwa kujidhibiti kwenye boti, jambo lililosababisha ateleze na kuanguka majini.
Kulingana na Bw Ooko, marehemu aliugua ugonjwa wa kifafa.
“Alikuwa akinyosha mwili wake na kuelekea ukingoni mwa boti. Hatimaye alianguka na kuzama,” alisema Bw Ooko.
Wakati wa tukio hilo, Bw Ooko alisema alishindwa kumwokoa marehemu, licha ya kujaribu kumuokoa kwa kumshika mikono.
Alisema kuwa mikono yao yote ilikuwa imelowa na walishindwa kushikana kwa nguvu.
“Nilijaribu kuvuta nyavu tulizokuwa tukitumia kwenye boti kwa matumaini ya kumshika kabla hajazama zaidi, lakini haikusaidia,” alisema.
Wavuvi wengine waliokuwa karibu na eneo hilo walisikia kilio cha Bw Ooko na kufika katika sehemu hiyo huku wakianzisha msako wa kumtafuta mwenzao aliyekuwa ameanguka majini.
Walitupa nyavu zao ziwani kwa lengo la kumtoa Okombo, hadi mwendo wa Jumamosi alasiri walipopata mwili wake.
Msako huo uliendelea hadi alasiri ya Jumamosi ndipo mwili wake ulipopatikana.
Bw Ooko aliandikisha taarifa katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay kueleza jinsi ndugu yake alivyodondoka kutoka kwenye boti.
Kisa kingine sawia kiliripotiwa katika ufuo wa Kananga mwezi Januari, baada ya mvuvi kufariki akiwa peke yake kwenye boti.
Chifu wa Kata ya Arujo, Bw Bob Lango, alisema ziwa hilo limekuwa likishuhudia visa vya watu kuzama.
Alisema ni jambo la kusikitisha kwamba visa vyote vimekuwa vikihusishwa na wavuvi kushindwa kuvaa jaketi za kuokoa maisha.
Mwili wa Okombo ulipatikana akiwa amevalia fulana pekee.
Bw Lango alisema kuwa marehemu huenda asingefariki iwapo angevaa jaketi ya kuokoa maisha.
“Jaketi za kuokoa maisha zimetengenezwa kusaidia watu kuelea majini iwapo ajali itatokea. Ni kosa la wavuvi wenyewe kwa kutozingatia usalama wao,” alisema msimamizi huyo.
Baadhi ya wavuvi walidai kuwa gharama ya kununua jaketi hizo ni kubwa.
Bw Odoyo Bati, mvuvi katika ufuo wa Nyagina, aliiomba serikali ya Kaunti ya Homa Bay kusaidia jamii za wavuvi kupata jaketi za kuokoa maisha.
“Jaketi hizo zinaweza kutumiwa na kila mmoja kwa kuwekwa chini ya usimamizi wa kamati za usimamizi wa fukwe,” alisema.
Leave a Reply