
WAKENYA wanaopata huduma za matibabu katika hospitali za kibinafsi zinazohudumu maeneo ya vijiji na mijini watakosa huduma hizo kuanzia Jumatatu, Februari 24, 2024.
Hii ni baada ya uongozi Chama cha Hospitali za Mashinani (RUPHA) kuagiza kutoa huduma za dharura pekee na kwa wagonjwa waliokuwa wamejisajili kwa matibabu kabla ya agizo hilo kutolewa.
Wagonjwa wasiohitaji huduma za dharura na waliojiandikisha kwa bima mpya inayosimamiwa na Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) pamoja na walimu na polisi wanaofaidi kutokana huduma za Kampuni ya Usimamizi wa Dawa (MAKL) watalazimika kulipa pesa taslimu ili kupata huduma.
Chama hicho cha RUPHA pia kilisema kuwa wagonjwa ambao walikuwa wamelazwa kabla ya Jumatatu, Februari 24, wataendelea kupata huduma katika hospitali hizo chini ya masharti ya sasa.
Akiongea na Taifa Leo Jumapili, Mwenyekiti wa RUPHA Dkt Brian Lishenga alisema serikali haijajaribu kuwafikia kwa lengo la kushughulikia malalamishi yao ya kutaka SHA iwalipe Sh30 bilioni wanazodai serikali.
“Tumejaribu kufikia serikali. Niliongea na Waziri wa Afya na mmoja wa makatibu wa wizara. Waziri alisema kuwa atawasilisha suala hilo kwa rais lakini hatujui ni lini atafanya hivyo. Katibu huyo wa Wizara alisema wako tayari kuanza kuandaa taratibu za malipo tunayodai,” akasema Dk Lishenga.
Lakini mwenyekiti huyo wa RUPHA alielezea hofu kwamba japo shughuli za kuandaa madeni ambayo hayajalipwa zimeanza, wafanyakazi wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) iliyofutiliwa mbali wamefutwa, hali ambayo imechangia kupungua kwa wafanyakazi katika maeneo ya mashinani ambao watasaidia kuandaa hesabu hizo za pesa wanazodai.
“Hatuna mpango madhubuti na hatujafanya mazungumzo yoyote yanayoweza kuchangia kupatikana kwa mwafaka kuhusu masuala muhimu,” Dkt Lishenga akasema.
Mwenyekiti huyo aliambia Taifa Leo kwamba hadi wakati huu, hawajapata ahadi yoyote kuhusu malipo ya huduma kwa mpango wa bima ya walimu na polisi.
“Walisema kwamba wametoa kiasi fulani cha pesa kwa MAKL, lakini hawajalipa pesa tunazodai. Tunadai malimbikizi ya miezi 11. Hatuna habari kuhusu iwapo watalipa pesa hizo au la,” akasema Dkt Lishenga.
Katibu wa Wizara ya Afya Harry Kimtai alituma taarifa kwa vyumba vya habari Jumapili jioni akitoa wito kwa chama cha RUPHA kubatilisha agizo lake kwamba huduma za afya zisitishwe.
“Tunahimiza hospitali za kibinafsi kuendelea kutoa huduma ili Wakenya wasiteseke. Tunawahakikishia kuwa shughuli ya uthibitishaji na utayarishaji pesa ambayo hospitali hizo zinadai inaendelea,” akasema,
“SHA na Wizara ya Afya zinashirikiana kusaka fedha za kugharamia malipo hayo. SHA imejitolea kulipa madeni yote,” Bw Kimtai akaongeza.
-IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA
Leave a Reply