Ajira kupotea serikali ikiunganisha mashirika zaidi kuokoa pesa – Taifa Leo


SERIKALI inapanga kuyaunganisha mashirika zaidi ya serikali ambayo yanatekeleza majukumu sawa, miezi mitatu baada ya Baraza la Mawaziri kuamua kuyaunganisha mashirika 42.

Kamati ya Kiufundi ya Idara za Serikali (IGRTC) imetambua mashirika mengine zaidi ambayo majukumu yao yanafanana au yale ambayo majukumu yao yanaingilia kaunti.

Afisa Mkuu Mtendaji wa IGRTC Kipkirui Chepkwony amesema hatua hiyo inalenga kuharakisha kuhamishwa kwa majukumu yote yaliyogatuliwa hadi kwa serikali za kaunti.

Hata hivyo, kibarua sasa ni iwapo kaunti zina rasilimali na uwezo wa  kutekeleza au kusimamia majukumu hayo.

“Changamoto kuu ambayo itatukabili hapa mbele ni kuhakikisha kuwa kaunti zinatekeleza majukumu haya bila tatizo lolote baada ya kuzihamisha,” akasema Mwenyekiti wa IGRTC Kithinji Kiragu.

“Hata hivyo, kile ambacho kinafaa zaidi ni kuwa serikali kuu na ile ya kaunti zinafanya kazi pamoja hasa katika kusawazisha bajeti,” akaongeza Bw Kiragu.

Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo inalenga kumaliza mchakato wa kuhamisha majukumu na kuunganisha mashirika hayo kufikia mwezi ujao.

Hii itahakikisha kuwa mgao wa bajeti wa 2025/26 unajumuisha pesa za majukumu yaliyohamishwa kwa kaunti.

“Kwa hivyo tuna muda wa hadi Julai 1, 2025  jinsi ilivyokubali kuhamisha na kuhakikisha kuwa kila mtu anaelewa jinsi shughuli hizi zitakavyoendeshwa na athari ya kuhamishwa kwa majukumu hayo,” akasema Bw Chepkwony wakati wa warsha mjini Naivasha.

Bw Chepkwony alikuwa akiwazungumzia washikadau kutoka serikali ya kitaifa na ya kaunti ambapo alisema hoja kuu ni kuhakikisha kaunti zinapata ufadhili au mgao wa kutosha kusimamia majukumu yaliyohamishwa.

Mnamo Januari, baraza la mawaziri  liliidhinisha kupunguzwa kwa masharika ya serikali ambapo idadi yao ingepunguzwa kutoka 42 hadi 20.  Uamuzi huo wa baraza la mawaziri ulilenga kupunguza bajeti ya serikali ili majukumu yanayofanana yatakelezwa na shirika moja kuzuia ubadhirifu wa pesa.

“Mageuzi haya yatarahisisha utoaji wa huduma na kuzima mienendo ya mashirika kutegemea ufadhili wa Hazina Kuu pekee badala ya kujisimamia. Pia mianya ya ubadhirifu wa fedha au pesa kutengewa majukumu yanayofanana itazibwa,” ikasema taarifa kutoka baraza la mawaziri.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa mashirika tisa ya serikali yangevunjwa huku majukumu yao yakihamishiwa wizara mbalimbali. Mashirika mengine 16 ambayo majukumu yao yanatekelezwa na sekta ya kibinafsi nayo yangevunjwa kabisa.

Ingawa hivyo, serikali ilitoa hakikisho kuwa hakuna nafasi za kazi ambazo zingepotea. Kwa kuwa uhamisho wa majukumu hayo umeanza, inasubiriwa kuona jinsi kaunti zitakavyozisimamia.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*