PENALTI tata na kadi mbili nyekundu zilizotolewa na refa zilisababisha vifo 56 kufuatia vurumai zilizozuka wakati wa mechi kati ya Labe na wenyeji Nzerekore, nchini Guinea, Jumapili.
Mechi hiyo ya nuksi ilikuwa fainali ya mashindano yaliyoandaliwa kwa heshima ya Rais Mamady Doumbya. Rais Doumbya aliingia mamlakani kupitia mapinduzi Septemba 2021.
Katika mchuano huo refa alifanya maamuzi ya kutatanisha yaliyoudhi mashabiki wa Labe na wakaanza kumrushia mawe kwa hasira. Polisi walijaribu kutuliza hali kwa kurusha vitoa machozi upande wa Labe bila mafanikio.
“Fujo zilianza wakati refa alitoa uamuzi wa utata uliofanya mashabiki kuingia uwanjani,” mtu mmoja aliyeshuhudia kisa hicho aliambia wanahabari.
Mwingine akaongeza kupitia simu: “Mawe yalianza kutupwa kisha polisi wakaingia na kufyatua vitoa machozi kutawanya watu. Katika patashika na vuruumai zilizofuata niliona watu wakianguka chini, wasichana na watoto wakikanyangwa. Lilikuwa tukio bovu sana, la kutisha na kusikitisha.”
Video na picha katika mitandao ya kijamii zilionyesha umati wa watu ukijaribu kuruka ua, huku miili ikitapakaa sakafuni.
Shirikisho la Soka nchini Guinea (FEGUIFOOT) limetaja tukio hilo kuwa la uchungu mwingi na kuongeza kuwa soka inafaa kuunganisha mioyo na kuleta vichwa pamoja wala si kusababisha maafa na majonzi.
Inaaminika maelfu ya mashabiki walihudhuria mechi hiyo kati ya Nzerekore na Labe wakati wa fujo hizo. Upinzani unadai kuwa michuano hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni ya kupigia debe kiongozi wa kijeshi Doumbya anayemezea mate kuwania urais katika uchaguzi ambao utawala huo wa kijeshi haujasema utafanyika lini.
Jumatatu, kundi la upinzani la National Alliance for Change and Democracy pia lililimbikiza lawama kwa serikali kwa matukio hayo ya kusikitisha.
Miezi ya hivi majuzi, viongozi wa soka wamekuwa wakimulikwa. Mwezi Julai rais wa FEGUIFOOT, Aboubacar Sampil, alichunguzwa kwa madai ya ufisadi na ghasia katika soka.
Mmoja wa wafanyakazi wa shirikisho hilo alishutumu Sampil kwa kuchochea ghasia na kujaribu kushawishi marefa wakati wa mechi ambayo timu ya ASK, ambayo yeye ni mmoja wa wakurugenzi wake, ilikuwa ikipoteza 0-1 mikononi mwa Milo FC.
Milo FC ilikataa kuendelea na mechi na ikatatizika kuondoka uwanjani. Sampil pia amelaumiwa kwa kupuuza itifaki na kwa mapendeleo katika kupatiana kazi.
Waziri Mkuu Oury Bah ametuma risala za rambirambi kwa waliofiwa na kusema kuwa uchunguzi utafanywa kunasa wahusika. Aliahidi usaidizi wa kimatibabu na kisaikolojia kwa wale walioumia.
Leave a Reply