SASA ni wazi kwamba Kenya imeziambukiza majirani zake Tanzania na Uganda “ugonjwa” wa utekaji nyara wa watu wanaokisiwa kuwa wakosoaji wa serikali.
Hii ni kufuatia ongezeko la visa vya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kutekwa nyara kwa njia ya kutatanisha katika nchi hizo jirani.
Kisa cha hivi punde kilitokea Jumapili, Desemba 1, 2024 jijini Dar es Salam ambapo kiongozi wa vijana wa chama cha upinzani ACT Wazalendo, Abdul Nondo alitekwa nyara katika kituo cha mabasi ya uchukuzi wa umma.
Polisi walidai kuwa mwanasiasa huyo, ambaye hawakumtambua kama Nondo, alikamatwa majira ya asubuhi na watu wawili waliokuwa wakisafiri kwa gari jeupe aina ya “four-wheel-drive”.
Ameachwa ufuo wa Coco Beach
Hata hivyo, mwanasiasa huyo alipatikana Jumatatu, Desemba 2, 2024, asubuhi akiwa ameachwa katika fuo ya Coco Beach.
Naibu mwenyekiti wa chama chake, ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita alinukuliwa akisema kuwa Nondo alipigwa na kujeruhiwa na akakimbizwa hospitalini kwa matibabu.
“Mwenzetu alifunikwa uso na kuchapwa vibaya zaidi huku watu hao wakitishia kumuua,” Bw Mchinjita akanukuliwa akisema.
Polisi walitoa taarifa wakithibitisha kuwa mwanasiasa huyo alipatikana katika Coco Beach.
Walisema Nondo aliachwa katika ufuo huo na watekaji wake na akaomba usaidizi kutoka kwa mwendesha pikipiki aliyempeleka hadi afisi za chama chake.
“Kutoka hapo, viongozi wa chama walimkimbiza hospitalini kwa matibabu. Tunaendeleza uchunguzi na tutachukua hatua za kisheria,” msemaji wa polisi David Misime akasema Jumatatu asubuhi.
Kutekwa nyara kwa Nondo kunafuatia kisa kingine cha kutekwa nyara na kuuawa kwa mmoja wa maafisa wakuu wa chama kikuu cha upinzani mnamo Septemba mwaka huu.
Ali Mohamed Kibao ambaye alikuwa akihudumu katika Sekritariati ya chama cha Chadema, alikamatwa ndani ya basi moja la abiria, akacharazwa kikatili kabla ya kuuawa kwa kumwagiwa asidi.
Rais Samia Suluhu Hassan alishutumu kisa hicho na kuamuru uchunguzi ufanywe kubaini wahusika katika mauaji hayo ili wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.
Viongozi wakuu wa Chadema
Kando hayo , mnamo Agosti mwaka huu viongozi wakuu wa Chadema; mwenyekiti Freeman Mbowe, naibu wake Tundu Lissu na katibu mkuu John Mnyika walikamatwa na kuzuiliwa korokoroni kwa madai kuwa wanafanya mkutano bila kibali.
Mnamo Novemba 16, mwaka huu, kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda, Forum for Democratic Change (FDC), Kizza Besigye alitekwa nyara nchini Kenya kwa njia ya kutatanisha.
Ilisemekana kuwa Dkt Besigye alitekwa nyara katika jumba moja lililoko mtaa wa Riverside Drive, Westlands, Nairobi.
Mwanasiasa huyo, ambaye amewahi kuwania urais mara nne kumpinga Rais Yoweri Museveni, alikuwa amewasili Kenya kuhudhuria hafla ya kuzinduliwa kwa kitabu kilichoandikwa na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua.
Dkt Besigye alisafirishwa kwa barabara hadi Uganda ambako alizuiliwa katika gereza moja la jeshi jijini Kampala.
Baadaye alifunguliwa mashtaka kwa kosa la kupatikana na bunduki mbili na kupanga njama ya kuhujumu Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF).
Msemaji wa Polisi nchini Kenya Dkt Resila Onyango amekana madai kuwa Besigye alitekwa nyara Kenya.
“Hatuna habari zozoye kuwa mwanasiasa wa Uganda Kizza Besigye alitekwa nyara. Kutoweka kwake hakumaanishi kuwa ametekwa. Tumeanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo,” Dkt Onyango akasema.
Usaidizi wa polisi wa Kenya
Hata hivyo, Waziri wa ICT na Mwongozo wa Kitaifa Chris Baryomunsi alisema maafisa wa usalama wa Uganda hawangemkamata Besigye bila usaidizi kutoka polisi wa Kenya.
Mnamo Oktoba 21, mwaka huu, serikali ya Kenya ilikubali kuwa iliwarejesha kwao raia wanne wa Uturuki walioripotiwa kutekwa nyara eneo la Lavington Nairobi.
Raia wa Uturuki waliotekwa nyara ni wafuatao; Mustafa Genç, mwanawe wa kiume Abdullah Genç, Hüseyin Yeşilsu, Necdet Seyitoğlu, Öztürk Uzun, Alparslan Taşçı, na mkewe Saadet Taşçı.
Watu hao waliingia nchini Kenya kama wakimbizi wakihofia maisha yao nchi mwao.
Kutekwa nyara kwa raia hao wa Uturuki na kurejeshwa kwao nyumba, kulishtumiwa vikali na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ikiwemo Amnesty International, tawi la Kenya.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Irungu Houghton alisema hatua hiyo ni kinyume cha sheria za humu nchini na zile za kimataifa.
“Isitoshe, hiyo ni ukiukaji wa haki za kimsingi za raia hao wa kigeni ambao walitorokea Kenya kwa usalama wao. Kuwarejessha Uturuki kwa nguvu ni kuwatumbukiza katika hatari tena,” akaeleza.
Tangu Juni mwaka huu wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z, visa vya watu kutekwa nyara na wengine kupatikana wameuawa vimekithiri zaidi nchini Kenya.
Wakosoaji wa serikali ya Kenya Kwanza
Waliolengwa zaidi ni wale ambao walisawiriwa kuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza.
Hata hivyo, alipofika mbele ya wabunge mnamo Novemba 7, 2024, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alikana madai kuwa polisi ndio wahusika katika visa hivyo vya utekaji nyara.
“Kama polisi, sisi huwa hatuteki watu nyara. Sisi huwakamata washukiwa wa uhalifu na kuwafungia katika vituo halali vya polisi. Kisha watu hao hufunguliwa mashtaka kortini kwa mujibu wa sheria,” akaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama, inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo.
Kanja aliiambia Kamati hiyo kwa tangu Juni mwaka huu, polisi imenakili visa 57 vya watu kutoweka, watu 22 wamepatikana wakiwa hai, wawili wakiwa wamekufa na 29 bado hawajulikani waliko.
Lakini katika ripoti iliyotoa Novemba 20, 2024, Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ilinakili visa 74 vya watu kutekwa nyara tangu mlipuko wa msururu wa maandamano ya Gen Z.
Leave a Reply