Siri ya ukuzaji miti kuimarisha kilimo na kuhifadhi mazingira – Taifa Leo


JULIUS Waweru, 30 amekuwa katika shughuli za kilimo kwa miaka kadhaa akijitegea uchumi eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a.

Wito unaotolewa na serikali kuhusiana na upandaji miti ili kupiga teke athari mbaya ya mabadiliko ya hali ya anga, umekuwa kichocheo kikubwa kwake kupanua kilimo biashara.

Yeye ni mtaalamu wa kilimo na mwasisi wa kampuni ya Ukulima Modern Seedlings and Nurseries.

Shamba lake la miche ya miti mbalimbali, ikiwemo ya matunda, liko karibu na barabara kuu ya Thika – Nyeri – Marua Highway.

Anapopandikiza miche udongoni katika vitalu, Waweru huelewa fika juhudi zake ni za kuokoa ulimwengu kutokana na ukame pamoja na kuunda mfumo thabiti wa utoshelevu wa chakula.

Kila harakati yake shambani inalenga kutimiza himizo la mpango anaouthamini kwa jina Trees for Food and Nature initiative.

Hii ina maana kuwa Ukulima Modern Seedlings and Nurseries hujikita katika upandaji wa miti kupata chakula na pia kuhifadhi mazingira.

“Azimio langu limejikita ndani ya shauku ya upanzi wa miti kwa lengo kubwa la kutunza mazingira na kustawisha kilimo kwa njia endelevu,” anafichua.

“Nimefaulu kuunganisha wanarika watano kujiunga nami kufanikisha kilimo biashara,” Waweru anasema.

 

“Kufikia sasa, tumeweza kukuza miche aina tofauti – kujumuisha miti ya matunda na ile ya kiasili. Kwa kila miti 10 ya matunda, sisi hupanda mti mmoja wa kiasili.”

Miongoni mwa miti inayopandwa hapa kuna michungwa, migomba, mipapai, miparachichi, miembe, tufaha, makadamia na mikarakara.

Vile vile, Waweru huuza miche ya viungo vyenye tiba kama vile lemon grass na oregano.

Isitoshe, ili kutosheleza mahitaji ya wateja mbalimbali, mkulima huyu huandaa miche ya miti ya urembo na matumizi mengine katika mazingira.

“Pia tunauza miti ambayo husaidia kuweka kivuli; inaweza kuwa ya kisasa (kigeni) ama ya kiasili,” anaeleza.

Kujitolea kwake kumemwezesha kufaidika na mitandao ya kijamii ili kijivumisha na kufikia wateja wengi pamoja na kuhamasisha watu kupanda miti.

 

“Nimetumia majukwaa yangu ya mitandao ya kijamii kuhimiza watu wapande miti. Hii imeongeza mawanda ya soko langu hadi nje ya kaunti. Kwa hakika, wateja wangu wengi wametoka katika mitandao hii,” Waweru anakiri.

Bidii yake imemvunia ushirikiano muhimu na mashirika ya serikali na yale ya kibinafsi.

Mojawapo ya asasi ambazo zimemshika mkono ni serikali ya Kaunti ya Murang’a ambayo imemtumia kupiga jeki miradi ya utumizi wa ardhi kwa njia endelevu.

“Tunahimiza kuwepo kwa mitindo ya kilimo ambayo inahuisha ardhi ili kuzalisha chakula na kutunza mazingira,” anadokeza.

 

“Kupitia usambazaji wa miche kusaidia wakulima ili watunze udongo na chemchemi, juhudi zetu zinalenga kukuza uendelevu wa kudumu.”

Kampeni za serikali kuhamasisha wananchi wapande miti kukabili athari hasi ya mabadiliko ya tabianchi, zimechochea ukuaji wa biashara yake.

Ameshuhudia haya baada ya idadi ya miche anayosambaza, kuongezeka kila kuchao.

Alipata utaalamu wa kilimo alipokuwa mwanafunzi katika kituo cha mafunzo cha Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo nchini (KALRO).

Nafasi hii ilimjengea msingi wa kupanua mtandao wa wateja baadaye alipoanza mradi wake mwenyewe.

Zaidi ya hayo, Waweru hupanda mboga na stoberi shambani mwake ili kuzidisha mazao na mapato.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*