Sababu za wanaharakati kutaka Kihika atupwe gerezani – Taifa Leo


KUNDI moja la wanaharakati linataka korti iamuru Gavana wa Nakuru Susan Kihika atupwe ndani miezi sita kuhusiana na uchafuzi wa Ziwa Nakuru.

Shirika la Baboon Project Kenya liliambia Jaji Anthony Ombwayo kuwa Bi Kihika na Meneja Mkurugenzi wa huduma za usafi James Ng’ang’a, walipuuza amri ya korti iliyotolewa Septemba 2024.

Kundi hilo linasema uchafu wa viwanda hutupwa kila kuchao katika ziwa licha ya kuwepo kwa amri ya kusitisha tabia hii.

“Licha ya kujua kuna amri ya korti, washtakiwa na maafisa wao, maajenti na watumishi wamedinda kuiheshimu. Wameendelea kumwaga takataka, kemikali ya sumu na uchafu wa viwanda ziwani,” Wakili Kirui Kiprotich aliambia korti.

Kupitia Katibu wa Kaunti, Bw Samuel Mwaura, Bi Kihika alipinga kesi hiyo akisema si jukumu lake kusimamia Shirika la Huduma ya Maji ya Nakuru.

“Ninapinga kuwepo katika rufaa hii. Mlalamishi hajathibitisha na hawezi kuthibitisha kuwa Gavana amekosa kuheshimu mahakama,” Bw Mwaura akasema katika kesi ambayo itaamuliwa Januari 31.

Katika uamuzi wa Septemba 24, Jaji Ombwayo alibaini kuwa kuna ripoti iliyoangazia kudorora kwa usafi wa maji kwa sababu ya uchafuzi wa Ziwa Nakuru.

Hali hii imetokana na majitaka, maji ya mvua yanayosomba uchafu hadi majini na taka za viwanda.

“Korti hii imeamua kuwa rufaa hii ina usahihi kwa sababu washtakiwa (serikali ya kaunti) ina jukumu kubwa katika usimamizi na utunzaji wa mazingira (Ziwa Nakuru), jukumu ambalo wamepuuza,” jaji wa  Mahakama ya Mazingira na Ardhi alisema.Jaji huyo alitoa amri ya kulazimisha serikali ya kaunti na shirika la maji kutafuta suluhu mbadala ya kutupa kemikali ya sumu na uchafu wa viwanda.

Walinda mazingira walisema wachafuzi hawa wanafanya hivi kwa makusudi na wanaendelea kuchafua ziwa hilo, kitendo ambacho kinahatarisha afya ya wanyamapori.

Mkurugenzi wa kundi hilo Simon Gichohi Mbuthia anaamini serikali ya Kaunti ya Nakuru ina jukumu kubwa kufuata ilani na ripoti kuhusu uchafuzi wa ziwa.

Alitaja ilani mbalimbali pamoja na ripoti ya Taasisi ya Maji na Uvuvi nchini iliyobaini kuwa kuna sumu na uchafu mwingi katika ziwa Nakuru.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*