
KUNDI la wanaharakati sasa linamtaka Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula afungwe miezi sita kwa kukiuka amri ya korti kuwa Muungano wa Azimio la Umoja ndio unastahili kushikilia upande wa wengi Bungeni.
Wanaharakati hao pia wanataka mahakama irekebishe amri ya Februari 7, 2025 iliyoamuru kuwa Bw Wetang’ula hawezi kuendelea kuhudumu kama spika iwapo ataendelea kuwa kiongozi wa Ford Kenya.
Katika uamuzi wao, majaji walitoa uamuzi kuwa Bw Wetang’ula hawezi kutekeleza jukumu lolote la kikatiba kama spika iwapo ataendelea kuwa kiongozi wa chama cha kisiasa.
Aidha, wanaharakati hao wamewasilisha kesi katika Mahakama ya Milimani wakitaka korti iharamishe uamuzi wa Bw Wetang’ula wa Februari 12, 2025.
Kwenye uamuzi huo, Bw Wetang’ula alisema Muungano wa Azimio ndio mrengo wa wachache huku ule wa Kenya Kwanza ukisalia mrengo wa wengi.
Wamesema Bw Wetang’ula hawezi kutoa uamuzi kama huo akiwa spika na wakati uo huo akiwa kiongozi wa Ford Kenya.
“Tunaomba korti itoe uamuzi kuwa vikao vya bunge vinavyoongozwa na Wetang’ula visitambuliwe kisheria akiendelea kuwa kiongozi wa Ford Kenya na Kinara wa Kenya Kwanza,” ikasema nakala ya kesi ambayo wamewasilisha.
Mnamo Februari 7, Bw Wetang’ula alisema Kenya Kwanza ndio upande wa wengi ikiwa na wabunge 165 huku muungano wa Azimio ukiwa na wabunge 154.
Wanaharakati wanasema uamuzi huu unavuruga na kuzima uamuzi wa mahakama.
Kupitia wakili wao Kibe Mungai, Bw Wetang’ula alistahili kutii uamuzi wa mahakama na kutangaza Azimio kama mrengo wa wengi kwa kuzingatia matokeo ya uchaguzi wa mnamo 2022.
“Kwa mujibu wa kesi, spika alistahili kutekeleza uamuzi wa korti kwa kuhakikisha kuwa Azimio inachukua mrengo wa wengi baada ya uamuzi wake wa Oktoba 6, 2022 uliokosa kutambua Azimio kama mrengo wa wengi,” akasema Bw Kibe.
Wakili Kibe amesema uamuzi wa spika wa kutumia maelezo kutoka afisi ya msajili wa vyama ili Kenya Kwanza isalie mrengo wa wengi ni kukiuka amri ya korti na uamuzi wake.
“Mahakama inastahili kuondoa uamuzi usiozingatia sheria wa spika uliotolewa Februari 12, 2025,” akasema Bw Kibe ambaye rufaa yake inasubiri kusikilizwa.
Leave a Reply