Zaidi ya 7,000 wahofiwa kuuawa DRC tangu Januari huku hali ikiendelea kuzorota – Taifa Leo


GENEVA, USWIZI

ZAIDI ya watu 7,000 wameaga dunia tangu Januari kutokana na mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Waziri Mkuu wa DRC Judith Suminwa, Jumanne aliambia mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa linalosimamia haki za binadamu jijini Geneva wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa hali ya usalama nchini humo inaendelea kuzorota.

Kwa mujibu wa Suminwa, karibu vifo 3,000 viliripotiwa Goma huku wengine zaidi ya 450,000 wakiachwa bila makao. Hii ni baada ya kambi 90 za waliokuwa wamehama makwao kuharibiwa.

Tangu Januari, kundi la M23 limekuwa kwenye vita vikali mashariki mwa DRC na limefanikiwa kutwaa miji ya Goma na Bukavu na maeneo mengine yenye utajiri wa madini.

Serikali ya DRC imeshutumu M23 na kudai kundi hilo linafadhiliwa na serikali ya Rwanda kusambaratisha udhabiti wa serikali ya Rais Felix Tshisekedi.

Hata hivyo, Rwanda imekanusha madai ya DRC, Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi kuwa inaunga mkono wapiganaji wa M23 na imekuwa ikifadhili mapigano.

Suminwa alitaka mataifa mengine kuchukua hatua na kuwekea Rwanda vikwazo, akisema kumekuwa na mauaji na watu kulazimishwa kuhama makwao.

“Ni vigumu sana kueleza kilio cha mamilioni ya watu ambao wameathirika na vita hivyo,” akasema.

Mkuu wa UN Antonio Guterres aliyehudhuria mkutano wa Geneva, alisikitika kuhusu yanayoendelea DRC akiyataka mashirika ya haki ulimwenguni yasimame dhidi ya dhuluma ambazo zinaendelezwa dhidi ya raia DRC.

“Iwapo hili suala la uvunjaji wa haki halitatuliwa, mambo yatakuwa mabaya zaidi,” Suminwa akasema.

Zaidi ya watu 400,000 wametorokea Burundi ambayo ni kati ya nchi tisa zinazopakana na DRC ndani ya wiki mbili vita vinapoendelea kuchacha mashariki mwa taifa hilo.

Suminwa alionya kuwa hali mbaya ya usalama kisha shughuli za M23 na baadhi ya makundi yaliyojihami yanaweza kuathiri pia udhabiti na amani kwenye mataifa jirani.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*