Amini usiamini, anachosema Wamunyoro ndicho kilichoko ‘kwa ground’ Mlimani – Taifa Leo


UNAMWAMINI Riggy G? Hili si swali la kukunia kichwa, naamini umejibu mara moja, ila kimya-kimya.

Kutokana na uwazi wa mlalamishi huyo kutoka janibu za Mlima Kenya, maswali yanayomhusu yanajibika kwa wepesi.

Wapo wanaompenda kwa uwazi wake, hasa katika kutema ukweli usiochujwa, na pia wapo wanaomchukia kwa kutoboa mambo akatia kitumbua cha watu mchanga.

Majibu yoyote yanayotolewa kuhusiana naye hutegemea mtu binafsi anaunga mkono upande gani kisiasa, hasa wakati huu ambapo tunashuhudia siasa mseto.

Unadhani siasa zetu si mseto? Ukiulizwa kinara wa upinzani rasmi ni nani utajibuje? Najua umesema RAO, halafu ukakumbuka juzi umemwona Ikulu akilimbikiziwa sifa furifuri, kwa hivyo huna hakika.

Kila Mkenya amekanganyikiwa; hata bungeni huwezi kujua ni nani anayepiga kura upande gani kwa sababu pande zote zimetokea kupendana sana.

Unapaswa kujanjaruka! Wakati wowote unapowaona wanasiasa wa serikali na upinzani wakikumbatiana na kula sinia moja, jua wewe ndiwe pilau, hata ikiwa ‘Pilau Njeri’, ya viazi na mbaazi.

Unanyofolewa kama kuku, lakini huhisi chochote kwa kuwa pesa zako ziko Nairobi, nawe unalaza damu kijijini. Umemwachia fisi kazi ya kutunza mfupa, mbwa yuaja eti. Utakufa njaa.

Turejee kwa Riggy G. Nina changamoto moja kwako; haiwezekani kwamba unamwamini mwanakijiji huyo wa Wamunyoro wakati anaposema mambo unayokubaliana nayo pekee.

Kuwa muungwana, utikise kichwa na kusikiliza anaposema mambo usiyopenda pia kwani huo unaweza kuwa ndio ukweli. Ukweli mchungu tangu hapo.

Juzi amesema kitu nikajikuna kichwa kidogo… Kwamba RAO akitaka kuwa rais wa Kenya atengane na Zakayo, ajiunge na kundi lake!

Hicho kinasikika kama kichekesho cha mwaka, lakini, amini usiamini, nilikisikia nilipozuru mlimani Disemba mwaka jana.

Huenda humpendi RAO, hivyo umeapa ‘hata kwa dawa!’ Huenda humwamini Wamunyoro, labda umempuuza ‘danganya toto jinga’.

Lakini ukweli ni kwamba mazungumzo ya kumfanya RAO rais wa muhula mmoja kuanzia mwaka 2027 yanaendelea miongoni mwa viongozi wa Mlima Kenya.

Kosa la Riggy G ni kutoboa siri kabla ya wananchi wa kawaida kusadikishwa kukariri ‘RAO tosha!’

Huenda Riggy G amejikwaa ulimi, kwa kuwa pale mlimani maamuzi muhimu kama hayo hutoka kwa wakazi wa tabaka la chini, na huenda wakamkataa RAO, lakini huo ndio ukweli.

Viongozi wa Mlima wanatafuta mtu yeyote, hata RAO, wa kumwondoa Zakayo Ikulu, lakini raia wa kawaida bado hawajakubali kuwa RAO ni ‘mtu yeyote’.

Watakapoamua utajua.

Usijali kuhusu Wiper na wengine wanaoota eti watalala Ikulu siku moja; mwamuzi wa mbeba mwenge wa kundi hilo ni mkulima mdogo wa mlimani.

Hata hivyo, jua hili kwanza: Wamunyoro ndiye msemaji wa viongozi wa Mlima wakati huu; kila neno analosema, hata likiwa tusi, unapaswa kulizingatia kwa makini. Lina siri.

[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*