Wabunge kufuta kanuni zilizoweka ada ya vitambulisho Kindiki alipokuwa wizara ya Usalama – Taifa Leo


WABUNGE watabatilisha kanuni zinazolenga kuweka gharama kubwa ya kupata na kubadilisha kitambulisho cha kitaifa pamoja na usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kwa sababu ya umma kutoshirikishwa na kwamba zimegubikwa na makosa.

Mbunge wa Ainabkoi, Bw Samuel Chepkong’a ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Bunge la Kitaifa, alitoa msimamo wa kamati hiyo kwa Katibu wa Uhamiaji Julius Bitok wakati wa kikao na kamati hiyo Jumatano kufuatia malalamishi kutoka kwa wanachama wa kamati kuhusu ada hizo.

Bw Chepkong’a alimweleza Katibu Bitok kwamba Maisha Namba, kitambulisho ambacho Serikali inapanga kuzindua haijakitwa katika kanuni.

Kanuni za Usajili wa Watu (Marekebisho), Kanuni za usajili wa Kuzaliwa na Vifo (Marekebisho) zilichapishwa na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Ndani Prof Kithure Kindiki na zikaanza kutumika mara moja na kusababisha taharuki miongoni mwa Wakenya.

Jumatano, Bw Chepkong’a hakusita kumwambia Bw Bitok kwamba atahitaji kuchapisha upya kanuni hizo kwani ni vigumu kuzitekeleza katika hali yake ya sasa.

“Unaweza kufikiria kubatilisha kanuni hizi. Makosa ni mengi mno,” akasema Bw Chepkong’a na kuongeza kuwa stakabadhi zilizowasilishwa kwa kamati hiyo kama ushahidi kwamba kanuni hizo zilitekelezwa kwa ushirikishaji wa umma hautoshi.

“Katika masuala kadhaa ambayo tumezungumza ambayo ni ya msingi, utaweza kuhitaji kuchapisha tena na kubatilisha yale uliyotoa tayari, kwa sababu ni vigumu kufikia lengo lililokusudiwa,” Bw Chepkong’a aliongeza.

Maisha Namba ni kitambulisho chenye tarakimu 14 kinachotolewa wakati wa kuzaliwa na kutumika katika maisha yote ya mtu kama utambulisho wa kisheria na kuunganisha vitambulisho vingi kama vile nambari za Kadi ya Kitambulisho, Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA) Nambari ya Utambulisho Binafsi (PIN)) na cheti cha kuzaliwa kwa mfumo mmoja.

Hapo awali kitambulisho kipya kiligharimu Sh300, kabla ya kupunguzwa hadi Sh100 na baadaye Sh50 kabla ya malipo ya ombi kuondolewa chini ya utawala wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Chini ya Kanuni za Usajili wa Watu (Marekebisho) kupata au kubadilisha kitambulisho kunagharimu Sh1,000.

Kanuni za Usajili wa Kuzaliwa na Vifo (Marekebisho) zinapendekeza Sh1,000 kupata cheti cha kuzaliwa na kifo na kufanya marekebisho katika cheti cha kuzaliwa au kifo.

Awali huduma hizo zilitolewa bila malipo.

Katibu Bitok alitetea kuongezwa kwa ada hizo akisena kuwa ni muhimu kwani ziliongezwa mara ya mwisho miaka 36 iliyopita.

“Baadhi ya ada zilizopendekezwa pia ni muhimu ili kupunguza ulaghai na kuwa na maelezo ambayo ni sahihi. Pia ni suala la usalama wa taifa,” alisema Katibu Bitok.

Hata hivyo, wanakamati Lenguris Pauline (Mbunge wa Kike wa Kaunti ya Samburu), Komingoi Kirui (Bureti) na Charles Mamwacha (Bonchari) walipinga mapendekezo ya nyongeza ya ada, wakisema kuwa ni mzigo zaidi kwa Wakenya ambao tayari wametozwa ushuru kupita kiasi.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*