VIONGOZI wa ODM ambao wamekuwa wakijitapa serikalini wanafanya hivyo kumfurahisha Rais William Ruto ili kuhakikisha eneo la Mlima Kenya linaendelea kutengwa kwenye uongozi wa nchi.
Waziri wa Madini Hassan Joho, John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi (Kawi), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo-ndogo) na Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed ni kati ya wanasiasa wa ODM ambao wamekuwa wakizungumza vibaya mno baada ya kuingizwa serikalini.
Bw Joho aliyatoa matamshi kuwa baadhi ya wanasiasa ambao wanapinga utawala wa sasa na kuchochea wananchi waivuruge hata kupitia mitandaoni hawakufanya hivyo walipokuwa serikalini.
Matamshi haya bila shaka yalimlenga aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwa alihudumu serikalini kwa muda wa miaka miwili kabla ya kuondolewa na mabunge ya seneti na kitaifa.
Kuondolewa kwa Bw Gachagua kulitokana na hatua yake ya kufarakana kisiasa na Rais William Ruto. Bw Gachagua amefaulu kuteka Mlima Kenya kisiasa na hata uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki hauonekani kama uliomtikisa kisiasa.
Hili ndilo linahofisha ODM na lengo lao ni kupiga kelele zaidi ili Rais Ruto aendelee kufumbika macho kuwa hata kama amepoteza Mlima Kenya, ngome za kisiasa za Raila bado zitamuunga mkono mnamo 2027.
ODM wanajua kuwa hawakuunda utawala wa sasa na watafanya kila jambo kurindima ngoma ya Rais Ruto ili wasiondoleke serikali. Baadhi ya viongozi wa chama hata wamekuwa wakidai kuwa eneo la Mlima Kenya linasubiri tu waondoke kisha lirejee serikalini.
Hata hivyo, Rais anastahili kufahamu kuwa kujaza pengo la Mlima Kenya ambalo lilimpa karibu nusu za kura alizopata katika uchaguzi mkuu uliopita si rahisi.
Rais anastahili kuwashinikiza mawaziri hawa wasimsujudu tu bali wakati wa usajili wa wapigakura, wanastahili kuhakikisha kuwa watu kutoka ngome zao wanajisajili kwa wingi.
Leave a Reply