TANGU kuzaliwa kwake miaka 18 iliyopita, Wesley Baraka Baya amekuwa akitamani sana kwamba ipo siku moja atahudumia taifa la Kenya kama mmoja wa maafisa shupavu wa Jeshi la Ulinzi (KDF).
Hata hivyo, kinachomkula akili na kumkeketa maini kila kuchao ni hali yake ya afya.
Bw Baraka alizaliwa akiwa na virusi vya HIV, jambo ambalo kila akilifikiria, hasa kuhusiana na ndoto yake ya kuwa mwanajeshi, humkosesha usingizi.
Bw Baraka alizaliwa Aprili 23, 2006 katika kijiji cha Sabasaba, tarafa ya Hindi, Lamu Magharibi.
Wazazi wake, Peter Baya Wanje na Bi Nancy Auma Owira, walikuwa tayari wanaugua Ukimwi wakati wakimzaa Bw Baraka.
Babake, Bw Wanje, alikuwa akihudumu kama afisa wa polisi wa utawala (AP) kabla kufariki 2008, mwaka mmoja na nusu baada ya Bw Baraka kuzaliwa.
Alivyohimizwa kumeza dawa
Bw Baraka anasema licha ya kujipata akihimizwa na mamake kumeza dawa fulani kila siku katika maisha yake ya utotoni, katu hakufahamu bayana sababu zilizopelekea yeye kuendelea kutumia vidonge hivyo hadi alipotinga miaka saba.
“Katika udogo wangu, nilijipata tu nikimeza dawa bila kufahamu kwa nini. Ila nilipofikia miaka saba, nilihisi mambo hayako sawa. Hapo ndipo nilipata ujasiri wa kumuuliza mamangu sababu za mimi kumeza vidonge hata mara nyingine nikiwa si mgonjwa.
“Mamangu alinikalisha chini na kunieleza kinagaubaga kwamba nilizaliwa na Ukimwi na kwamba ni vyema nitumie dawa siku zangu zote ilmuradi niyamudu maisha,” akasema Bw Baraka.
Baada ya hapo, Bw Baraka anasema hakushtuka ila alijikubali na hata kumshukuru mamake kwa kuwa wazi.
Bw Baraka alianza kuyatazama maisha kwa njia tofauti kinyume na waja wengine ambao punde wanapojitambua kuugua Ukimwi wao hukata tamaa ya kuishi.
“Kuna watu ambao punde wanapojipata wakiugua Ukimwi wao hujiua. Wengine hukabiliwa na msongo wa mawazo kiasi kwamba hujiingiza katika anasa na uraibu wa pombe, dawa za kulevya na wanawake.
“Mimi nilifahamu kuwa Ukimwi kamwe siyo hati ya kifo. Nilijikaza kutia bidi maishani. Kwa sasa nikiwa umri wa miaka 18 nimejitahidi kusoma na kufikia mwaka ujao ninaingia kidato cha nne,” akasema Bw Baraka.
Yeye ni mzawa wa pili katika familia ya watoto watatu. Mkubwa wake na mdogo wake, ambao wote ni wasichana, hawana virusi vya Ukimwi.
Unyanyapaa shuleni
Bw Baraka anaishukuru familia yake, ikiwemo mamake, Bi Nancy Auma Owira, na dada zake wote wawili kwa kumpenda na kushirikiana naye vyema licha ya hali yake ya kiafya.
Hata hivyo anasema kuishi na virusi vya Ukimwi si jambo rahisi, akitaja unyanyapaa kuwa kizingiti kikuu kinachowavunja moyo wengi wanapoishi na kutangamana na jamii.
Anasema katika kipindi chote cha miaka 18 ya kuishi na Ukimwi, ameshuhudia mengi, ikiwemo baadhi ya walimu wake ambao wanajua hali yake ya virusi ambao mara nyingine wamekuwa wakiwaonya wanafunzi wenzake kutoshikana naye eti sababu ni kuwa ana virusi vya Ukimwi.
“Kuna wakati ambapo baadhi ya wanafunzi walichapwa viboko na mwalimu fulani na kuonywa dhidi ya kushikana nami, sababu ikiwa ni kwamba nimeambukizwa Ukimwi. Ni suala ambalo mara nyingi hunisikitisha sana,” akasema Bw Baraka.
Azma ya kuwa mwanajeshi
Ila anasisitiza kuwa huku akitarajia kukamilisha masomo yake ya upili mwaka ujao, ndoto yake ya kujiunga na jeshi nchini itatimia.
Mara nyingi kumeshuhudiwa makurutu wakitemwa nje wakati wa shughuli za kusajili vijana kuingia jeshini kwenye sehemu mbalimbali za nchi kutokana na sababu za kiafya.
Bw Baraka anaomba kuwepo na mageuzi kwenye idara ya jeshi (KDF) yatakayowezesha wanaogua Ukimwi kupewa nafasi kuitumikia nchi yao.
“Sitarajii KDF kuua ndoto yangu eti sababu ni Ukimwi. Na ndiyo sababu serikali yetu tukufu itekeleze mageuzi yatakayopelekea wenye Ukimwi pia kutumikia nchi yao, hasa hizi kazi za jeshi. Ninapania kuwa afisa wa KDF,” akasema Bw Baraka.
Akitinga miaka 18, ambao ni umri wa mtu mzima, Bw Baraka pia matarajio yake maishani ni kupata mwenza atakayemwelewa, kumpenda na kumuenzi ili waweze kuanzisha familia pamoja.
“Niko na azma kwamba siku moja nipate mke wa kunipenda na kunikubali hali yangu jinsi nilivyo. Nataka hasa nishikane vyema na huyo mke nitapata ili tuzae watoto na kufuatilia vilivyo ushauri wa kiafya. Nitahakikisha watoto tutakaozaa wataishi bila kuambukizwa virusi vya Ukimwi,” akasema Bw Baraka.
Safari ya kumkuza kijana wake
Kwa upande wake, mamake Baraka, Bi Nancy Auma Owira, anasema safari ya kumkuza kijana wake haikuwa rahisi.
Bi Auma amekuwa mstari wa mbele katika kumtia moyo Bw Baraka kujikaza na kuishi vyema bila kufuata wayasemayo watu.
“Kijana wangu Baraka ndiye aliyenifanya kujua kwamba mimi pia nina virusi vya Ukimwi. Baada ya kumzaa, kijana alianza kuuguaugua. Nilipitapita hospitalini hadi pale tulipofanyiwa vipimo mimi, bwanangu na Baraka, hivyo kupatikana tuko na virusi vya Ukimwi.
“Mume wangu alikufa mwaka mmoja na nusu baada ya Baraka kuzaliwa. Kifo chake kilisababisha uchungu Zaidi na hali ngumu,” akasema Bi Auma.
Kwa sasa Bi Auma ni mmoja wa wahudumu wa afya ya jamii mashinani kaunti ya Lamu, akiwahimiza waja, hasa wale wenye virusi vya Ukimwi, kuzingatia tiba, lishe bora, kujipenda, kuzingatia siku zao za kutembelea kliniki na kumeza dawa ipasavyo ili waendelee kuishi vyema.
Ila anaomba serikali na mashirika yasiyo ya serikali kufika Lamu na kuwasaidia walioathiriwa na Ukimwi.
“Wengi wanaoishi na virusi wanatoka familia maskini. Tunahitaji misaada ili kumudu maisha yetu,” akasema Bi Auma.
Leave a Reply