MWAKA mmoja baada ya Padre Edwin Gathang’i Waiguru kuwashangaza Wakenya wengi kwa kufunga ndoa katika eneo la Kiambu, amefunguka na kueleza kuwa sababu kuu iliyosababisha kuasi upadre wa Kanisa Katoliki la Roma ambao aliutumikia kwa miaka kumi ni kutokana na msukumo wa maisha ya Kiafrika.
Katika mahojiano na Taifa Dijitali, Padre Waiguru alisema utoaji huduma za kanisa la Katolik la Waroma huko Haiti kulichangia pakubwa.
Hii ni baada ya kujitambulisha kuwa Mroma, wakazi wa eneo hilo wakibaki kushangaa.
“Ilinihuzunisha sana kujitambulisha kama kasisi wa Roma ilhali mimi ni Mwanaume wa Kiafrika. Nilivutiwa sana kujifunza kuhusu maana ya kuwa Mwanaume wa Kiafrika na mila zetu,” alieleza Padre Waiguru.
Baadaye alirejea kuendelea kuhubiri Amerika Kaskazini na Kusini na kuhisi kuwa na haja ya kuoa na kuwa na familia.
Padri huyo alifahamisha viongozi wake kuwa na matamanio ya kuwa na ndoa. Alisema kuwa alitumia njia ya kufunga ndoa ili kuepuka muda wa kusafiri kutokana na cheti chake cha usafiri kusalia na muda mfupi.
“Nilipokuwa kwenye misheni nchini Amerika, niliamua kuacha upadre baada ya kukutana na mwanamke mmoja. Tulifunga ndoa naye ili nipate muda wa kuishi pale,” alieleza Padre Waiguru.
Baadaye Padre huyo alijiunga na kanisa Kanisa Katoliki Charismatic ili kutuliza moyo wake. Alisema kuwa kufikia sasa kuna mapadre 12 ambao wana familia, naomba wakati ufike na kupewa fursa ya kuzungumzia hali yao.
“Natamani sasa wezangu 12 pia wapate nafasi ya kuweka mambo yao wazi. Natumai muda mwafaka utatimia ili wazungumzie kuhusiana na hali yao,” alisema Padre Waiguru.
Padre Waiguru, ambaye sasa anahudumu chini ya Kanisa Katoliki Charismatic, aliamua kurudi nchini mwaka 2021 baada ya kukutana na mwanamke aliyeuteka moyo wake.
“Niliporudi nyumbani baada ya kuacha upadre wa Kanisa Katoliki la Roma, nilitarajia kupokewa kwa baridi, lakini sivyo ilivyokuwa. Kutokana na hofu na umbali wa kijamii, watu hawakuwa wakinijadili sana, jambo lililonipa nafasi ya kutulia na kupanga maisha na mke wangu mtarajiwa,” alisema.
Baadaye aliamua kumuoa katika sherehe ya kitamaduni. Wapenda harusi leo walishuhudia harusi ya kipekee ambapo Padre Waiguru alifunga ndoa na Margaret Wanjira Githui katika hafla ya kifahari iliyofanyika Michael’s Pot Gardens huko Ikinu, Githunguri Oktoba 22, 2023.
“Nilibarikiwa tena kuwa kasisi wa Kanisa Charismatic na pia nikaidhinisha ndoa yangu. Nimefurahi sana, Mungu ametubariki na watoto watatu, na bado namtumikia Mungu kama kasisi,” alisema.
Kulingana naye, bado ni mtumishi wa Mungu na ni Mkatoliki, lakini anatofautiana na Kanisa Katoliki la Roma kwenye sakramenti ya ndoa ambapo makasisi wa Kanisa lake wanaruhusiwa kuoa.
“Kanisa la Katoliki la Roma hawaruhusu kabisa ndoa. Kanisa la Katoliki la Charismatic tunahubiri Yesu. Hiyo ndio tofauti pekee.”
Leave a Reply