HOFU ya kuzuka upya kwa uharamia katika pwani ya Somalia na Bahari Hindi imetangazwa baada ya shambulio la meli ya uvuvi ya China ya LIAONING DAPING 578 kutekwa nyara ikiwa na mabaharia 18 wiki hii.
Jeshi maalumu la kupambana na uharamia la Muungano wa Ulaya (EU) siku ya Alhamisi lilithibitisha kutekwa nyara kwa meli hiyo na maharamia waliojihami kwa bunduki aina ya AK47s.
“Jeshi la EUNAVFOR ATALANTA lilipata habari kuhusu utekaji nyara wa meli ya uvuvi na tunathibitisha mabaharia 18 wamo katika mikono ya maharamia hao lakini wako salama. Kikosi chetu kinawasiliana na vitengo tofauti ili kuokoa waliotekwa nyara,” EU ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Mtaalamu wa maswala ya ubaharia Pwani, Bw Andrew Mwangura, alisema tangu Novemba mwaka jana, meli 22 zimetekwa nyara jambo ambalo limezua hofu miongoni mwa vitengo vya usalama duniani kwani huathiri usafirishaji wa mizigo.
“Taarifa zinadhihirisha kuwa maharamia sita wakiwa wamejihami walishambulia meli hiyo miezi tisa baada ya kuteka nyara meli kubwa ya nchi ya Iran eneo la Jifle kusini mwa Somalia. Meli hiyo imefikisha meli 22 ambazo zimetekwa nyara, zingine zikiachiliwa huku kadhaa zikibaki mikononi mwa maharamia,” alisema Bw Mwangura.
Bw Mwangura alisema visa hivyo vimechangiwa na upungufu wa wanajeshi wa kupiga doria katika Bara Hindi kwani wengi walipekekwa kupigana na waasi wa Houthi wa Yemen.
Vikosi vya kimataifa vinavyoshika doria kwenye Ghuba ya Aden na Bahari ya Hindi vimerejea kwenye Bahari Nyekundu, na hivyo kupunguza kiwango cha ufuatiliaji katika maeneo ya kusini zaidi, na kuzua hofu ya kuongezeka kwa vitendo vya uharamia, ingawa idadi yao ilipungua zaidi tangu mwaka 2011 baada ya kuanzishwa ukaguzi wa kimataifa.
Kumekuwa na jaribio la kukwamisha biashara katika Ghuba ya Aden kwa kushambulia meli za mizigo tangu Novemba mwaka jana visa ambavyo vimelazimu meli nyingi kubadili mkondo kusafirisha mizigo maeneo mbalimbali duniani.
Leave a Reply