KIKOSI cha maafisa wa usalama kinachodumisha amani Haiti kimekanusha ripoti kwamba maafisa wa polisi wa Kenya wamewasilisha barua za kujiuzulu kwa kucheleweshewa mshahara.
Shirika la habari la Reuters liliripoti Ijumaa kwamba maafisa wa polisi 20, miongoni mwa 400 waliotumwa katika taifa hilo linalothibitiwa na magenge, walijiuzulu miezi miwili iliyopita kutokana na kucheleweshwa kwa mishahara.
Ripoti hiyo pia ilisema kwamba maafisa hao hawajapata jibu la barua zao na wanaendelea kuhudumu kulingana na maafisa watatu ambao waliomba kutotajwa majina kwa sababu hawaruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.
Lakini Kamanda wa kikosi hicho Godfrey Otunge alikanusha vikali madai hayo na kuyataja kuwa ‘ yasiyo sahihi na ni yenye nia mbaya’.’Ripoti hizo, ambazo awali zilihusishwa na Reuters, zilidai kutoridhika kwa maafisa wetu miongoni mwa waliotumwa Haiti. Kikosi kinakanusha madai haya, habari hizi si sahihi na zina nia mbaya,” Bw Otunge alisema.
Kulingana naye, maafisa wote wamepokea mishahara yao na marupurupu kamili ya kila mwezi, na hakuna afisa aliyewasilisha barua ya kujiuzulu kama inavyodaiwa.
Kikosi hicho kilisisitiza kuwa maafisa wake wanasalia ‘na ari ya juu na wamejitolea kikamilifu’ kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) katika juhudi zinazoendelea za kusambaratisha mitandao ya magenge na kurejesha utulivu nchini Haiti.
Leave a Reply